SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeibuka na kusema kuwa Klabu ya Yanga itakabidhiwa fedha zao za kuingia hatua ya makundi ya Caf mara baada ya kumalizika hatua hiyo na si sasa kama wadau wengi wanavyodhania kuwa watapata mara baada ya kuingia katika hatua hiyo.
Yanga imefanikiwa kuingia katika hatua ya makundi mara baada ya kuiondoa Wolaitta Dicha ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 2-1, na watavuna kiasi cha shilingi milioni 600 kama wakimaliza katika nafasi ya nne.
Aidha makundi ya michuano hiyo tayari yameshatangazwa juzi Jumamosi ambapo imepangwa Kundi D ikiwa ni pamoja na Gor Mahia ya Kenya, Rayon Sport ya Rwanda na USM Alger ya Algeria.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ephraim August, amesema kuwa, Yanga haiwezi kukabidhiwa fedha zake sasa kwa kuwa haijulikani itamaliza nafasi ya ngapi, kwani kadiri inavyomaliza nafasi za juu, ndivyo fedha zinavyoongezeka.
“Milioni 600 ambayo inatajwa Yanga kuzipata baada ya kuingia hatua ya makundi, iwapo watamaliza michuano hiyo wakiwa wa mwisho kwenye kundi lao na iwapo watapanda na kumaliza wa pili kutoka chini, watapata milioni 750 na wakipiga hatua na kumaliza wa tatu kutoka chini watapewa milioni 850.
“Bingwa katika michuano ya Caf anaibuka na kitita cha shilingi bilioni 2.8, mshindi wa pili bilioni 1.2 na nusu fainali atachukua bilioni 1,” alisema.
Aliongeza: “Caf hawawezi kutoa fedha sasa hivi kwa kuwa hakuna anayejua timu ipi itamaliza katika nafasi ya ngapi, na vilevile hawatoi kabla kwa kuhofia timu inaweza kutoshiriki michuano.”
No comments:
Post a Comment