Msafara wa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, Godfrey Mheluka, umeshambuliwa na wananchi katika Kijiji cha Kashanda, Kata ya Nyakahanga alipokwenda kufuatilia mgogoro wa wafugaji na wakulima.
Katika mashambulizi hayo, Diwani wa Kata ya Nyakahanga, Charles Bechumila (CCM), amejeruhiwa vibaya kwa mishale na kukimbizwa katika Hospitali Teule ya Nyakahanga kutibiwa na alifanyiwa upasuaji huku hali yake ikielezwa kuwa ni mbaya.
Ilidaiwa kuwa mkuu huyo wa wilaya alikwenda kijijini hapo kutoa tamko kuhusu mgogoro wa wakulima na wafugaji akiwa na msafara wa magari mawili.
Katika gari lake alikuwa amepanda na Katibu Tawala wa Wilaya (DAS), Innocent Msena na Ofisa Uhamiaji mmoja na askari polisi wawili.
Gari la pili katika msafara huo lilikuwa na Diwani Bechumila, maofisa tarafa wawili na waandishi wa habari wawili wa Redio Karagwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Ulomi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kuwa askari waliokuwa wameambatana na mkuu wa wilaya walilazimika kufyatua risasi juu kutawanya washambuliaji, huku msafara huo ukikimbilia katika magari ambayo yalikuwa yameachwa umbali wa mita 600.
Ilielezwa kuwa Mkuu wa Wilaya alikwenda kuwaagiza wakulima kuhama eneo hilo kuwapisha wafugaji na tayari agizo kama hilo alikwishalitoa awali akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha Juni 5, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment