Sunday, February 26, 2017

MAJAJI 3 KUAMUA KESI YA LEMA LEO

RUFAA ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) inatarajiwa kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Rufaa hiyo itasikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ambao ni Stella Mugasha, Kipenka Mussa na Bernard Luanda ambaye atakuwa mwenyekiti.

Kesi ya Lema ilikwama kutolewa uamuzi na Jaji Salma Magimbi, Januari 4, mwaka huu, baada ya Wakili wa Serikali, Innocent Njau, kuiomba mahakama hiyo kutoendelea na kesi hiyo kwa sababu wamekata Rufaa Mahakama ya Rufani, kupinga Jaji Dk. Modesta Opiyo, kumwongezea Lema muda wa siku 10 ili akate rufaa ya kunyimwa dhamana, nje ya muda.

Pia katika rufaa hiyo, itasikilizwa kesi ya mawakili wa Lema wanaopinga Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kukubali kumpa dhamana Lema.

Awali Jaji Salma Magimbi, alisema kwa kuwa upande wa Jamuhuri umekata rufaa hataweza kuendelea kutoa uamuzi wa rufaa ya Lema kulalamikia kunyimwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu mkazi Arusha.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilimpa dhamana Lema lakini kabla ya kusomewa masharti yake, mawakili wa Jamuhuri waliwasilisha kusudio la mdomo la kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa hakimu.

Jaji Dk. Opiyo alitoa uamuzi Desemba 20 mwaka jana wa kumwongezea Lema muda wa siku 10, ili akate rufaa ya kupinga kupewa dhamana bila masharti ya dhamana, na kutupa pingamizi mbili za wanasheria wa serikali, waliopinga kusikilizwa kwa rufaa hiyo kwa sababu ipo nje ya muda kisheria.

Jaji Dk. Opiyo alisema hoja hizo hazikuwa na mashiko.

Lema alianza kukaa mahabusu Novemba 2, mwaka jana, baada ya kukamatwa katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kusafirishwa kuletwa Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Arusha.

Novemba 8 alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha mbele ya Hakimu Desderi Kamugisha ambapo alisomewa shitaka la uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

Hakimu Kamugisha alikubali kutoa dhamana kwa Lema kwa madai kuwa sheria haizuii kutoa haki hiyo kwa mshtakiwa wa kesi ya uchochezi lakini kabla ya kutamka masharti ya dhamana, Mawakili wa Serikali, Paul Kadushi na Materius Marandu walidai wana nia kukata rufaa dhidi ya msimamo huo.

Kutokana na mawakili hao kusema hivyo, Hakimu aliamua kesi hiyo ibaki kama ilivyo, huku mtuhumiwa akisubiri maamuzi ya rufani ya Jamhuri katika Mahakama Kuu.

Jaji Dk. Opiyo alipotupa rufaa ya Jamhuri na kumpa Lema siku 10 zaidi ili akate rufaa ya kupinga kupewa dhamana bila masharti ya dhamana kwa kuwa hoja hizo hazikuwa na mashiko, mawakili wa serikali wakakata rufani Mahakama ya Rufani.

Tangu wakati huo Lema ameendelea kukaa mahabusu katika Gereza la Kisongo.

No comments:

Post a Comment