Saturday, May 6, 2017

YANGA MAJARIBUNI IKIIKARIBISHA PRISONS

NAHODHA WAKE NADIR HAROUB ''CANNAVARO".

IKIWA bila na nahodha wake Nadir Haroub ''Cannavaro" kikosi cha mabingwa watetezi Yanga, wanatarajia kutupa karata muhimu watakapoikaribisha Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga itashuka katika mechi ya leo ikiwa na kumbukumbu ya kuwafunga Prisons mabao 3-0 katika mechi ya hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la FA na goli 1-0 walipokutana Mbeya katika mchezo wa mzunguko wa kwanza.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema kuwa wamejipanga kucheza kwa tahadhari kwa sababu Prisons ni moja ya timu nzuri na zinazoleta ushindani kwenye ligi hiyo inayoshirikisha klabu 16. Mwambusi alisema wachezaji wao wataingia uwanjani kwa kasi ya juu na kuelekeza kuwa kwao hakuna mechi ndogo au rahisi.

"Tutaingia uwanjani kwa ajili ya lengo moja la kuondoka na pointi tatu, ushindi utatuweka salama kwenye mbio za ubingwa, hiyo ndiyo nafasi pekee tuliyonayo ili kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani, tunajua Prisons ni timu ngumu na wao wataingia uwanjani kusaka rekodi na pointi zitakazowaweka kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi," alisema kocha huyo.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, aliwataja wachezaji wawili ambao watakosekana katika mechi hiyo kuwa ni nahodha Cannavaro ambaye ana kadi tatu za njano la mshambuliaji Donald Ngoma ambaye amekwenda Afrika Kusini kupata matibabu.

Kocha wa Prisons, Abdallah Mohammed, alisema jana kuwa kikosi chake kimejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo na ametumia muda wa mapumziko wa wiki moja kurekebisha makosa waliyofanya katika mechi iliyopita dhidi ya mabingwa hao watetezi.

Mechi nyingine za ligi hiyo zinazotarajiwa kufanyika leo ni kati ya Toto Africans dhidi ya JKT Ruvu wakati Ruvu Shooting itawakaribisha Kagera Sugar, Majimaji ikiwavaa Mwadui FC na Azam FC ikicheza na Mbao FC, mchezo pekee utakaofanyika kuanzia saa 1:00 usiku.

No comments:

Post a Comment