Wakati Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) likijipanga kuikatia umeme
Zanzibar kama alivyoagiza Rais John Magufuli, SMZ inajipanga kuzungumza
na shirika hilo ili kuona namna ya kulipa.
Alipotafutwa kwa simu jana kuzungumzia utekelezaji wa agizo hilo,
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka alisema yupo safarini na
hakuzungumza kutokana na mawasiliano kuwa mabaya.
Baadaye mwandishi wetu alimtumia ujumbe mfupi, lakini Dk Mwinuka hakujibu.
Baada ya kukwama kupata maelezo ya Dk Mwinuka, mwandishi wetu alimtafuta
kwa simu, Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji ambaye alisema
shirika hilo litatekeleza agizo la Rais kama alivyoagiza.
“Rais ametoa kauli na kuagiza… lazima tutekeleze,” alisema Muhaji ambaye hakubainisha siku ya kuanza utekelezaji wa agizo hilo.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ,
Mohamed Aboud Mohamed alipoulizwa kuhusu deni hilo, alisema wamejiandaa
kufanya mazungumzo kati ya mawaziri husika wa pande mbili za Muungano
kuona namna wanavyoweza kufanikisha ulipaji wa deni hilo.
“Lengo letu ni kulipa deni lote kwa sababu ukidaiwa lazima ulipe. Tupo
tayari kulipa ndiyo maana tumeanza kufanya mazungumzo na wenzetu wa
Tanzania Bara, ili kuona namna tunavyoweza kukubaliana juu ya Shirika la
Umeme Zanzibar (Zeco) kulipa hatua kwa hatua ili kumaliza deni lote,”
alisema.
No comments:
Post a Comment