Thursday, August 9, 2018

COASTAL UNION YAJIVUNIA ALI KIBA

BAADA ya kurejea tena katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Coastal Union ya jijini Tanga imejipanga kufanya vizuri katika msimu ujao wa ligi hiyo ambayo inatarajiwa kuanzia Agosti 22, mwaka huu, huku ikiweka matumaini makubwa kwa mshambuliaji wao, msanii Alli Kiba.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda alisema anajivunia wachezaji aliowasajili katika msimu huu ambao mmoja wao ni msanii maarufu wa Bongo Flava nchini, Kiba, kuwa wamejiandaa kupambana kuhakikisha wanatwaa ubingwa.

Mgunda alisema kikosi chake kina wachezaji wengi vijana ambao wana nguvu na uwezo wa kupambana na wapinzani huku akiongeza kuwa hakuna timu wanayoihofia.

Kocha na mchezaji huyo wa zamani wa Coastal Union, alisema pia wamejipanga kucheza mechi nyingine za kirafiki tatu kabla ya kuanza kwa ligi ili kutoa nafasi kwa kila mchezaji kuonyesha alipofikia na kupata kikosi cha kwanza ambacho ni imara.

"Tunaendelea vizuri na mazoezi, nina matumaini makubwa sana na vijana wangu, hata hao waliosajili wachezaji wazee najua nao walianzia katika ujana, uzoefu haununuliwi, wana morali ya hali ya juu na wako tayari kupambana katika vita ya Ligi Kuu, " alisema kocha huyo.

Aliongeza kuwa Coastal Union imejipanga upya na itaanza msimu mpya kwa nguvu kuhakikisha haipotezi pointi katika mechi za awali kwa sababu haitaki kurejea ilikotoka na kujiweka kwenye hatari ya kushuka daraja kila wakati.

Mbali na Coastal Union, timu nyingine zilizopanda daraja ni pamoja na JKT Tanzania, African Lyon, KMC FC zote za Dar es Salaam, Alliance FC (Mwanza) na Biashara United ya Musoma mkoani Mara.

No comments:

Post a Comment