Chalamila alitoa msimamo huo jana alipokuwa anazungumza na viongozi wa dini na kueleza baadhi ya wanachama wa CCM Mkoa wa Iringa wanamshinikiza ajiuzulu, ili kukidhi matakwa ya utaratibu mpya wa chama unaotaka mtu mmoja kuwa na cheo kimoja.
Alisema ataendelea kuwa mwenyekiti mpaka Rais Dk. John Magufuli ambaye ndiye aliyemteua, atakapotoa maelekezo mengine.
“Baada ya kuteuliwa kuna baadhi ya watu walinifuata wakinitaka nijiuzulu nafasi ya uenyekiti, sasa ninachokijua ni kwamba Rais aliniteua kuwa Mkuu wa Mkoa akiwa anajua kuwa mimi ni mwenyekiti, hivyo naendelea kushika nyadhifa zote mpaka nitakapopata maelekezo mengine,” alisema Chalamila.
Katika hatua nyingine, Chalamila alisema kwa muda mrefu Jiji la Mbeya limekuwa halipati maendeleo kutokana na mwendelezo wa siasa chafu zinazoifanya serikali ishindwe kutekeleza baadhi ya miradi ya maendeleo.
Aliwataka viongozi wa dini kuisaidia serikali katika kuhubiri amani na kuwaelimisha vijana kufanya kazi kwa bidii badala ya kuendekeza vijiwe vya siasa zisizokuwa na manufaa katika maisha yao ikiwamo kukashifu vyama wasivyoviunga mkono.
Alisema katikati ya Jiji la Mbeya barabara ilitakiwa iwe ya njia nne na barabara ya mchepuko kutoka Uyole mpaka Songwe kwa ajili ya magari makubwa ya mizigo ilitakiwa iwe imejengwa, lakini siasa zimekuwa zikikwamisha.
“Hili ni jiji, lakini siku zote huwa najiuliza kuwa ni kweli serikali imeshindwa kujenga barabara ya njia nne, ni kweli serikali imeshindwa kujenga kilomita 40 barabara ya mchepuko na je, serikali imeshindwa kuukamilisha uwanja wa ndege wa Songwe na kuupa hadhi yake ya kimataifa?” Alihoji Chalamila.
“Ninachokiona hapa ni kwamba siasa ndiyo ‘zinatucost’ (zinatugharimu), mtu anaamua kurudisha nyuma mikono na kuacha aone tunavyofanya, lakini kwa sasa naona hali imeanza kuwa tulivu, mimi na katibu tawala tutamwandikia rais atusaidie baadhi ya miundombinu hii muhimu iboreshwe haraka,” alisisitiza.
Aliwaomba viongozi wa dini mkoani humo, kuendelea kuisaidia serikali kuwaelimisha vijana kuhusu mambo mbalimbali ya maendeleo na kuachana na siasa chafu ambazo hazina manufaa kwa sasa.
Aliwataka kuanzisha madarasa maalumu ya kuwafundisha vijana ujasiriamali kwenye maeneo yao ya kuabudia, ili wajikite kwenye shughuli hizo na kujiletea maendeleo.
Credit:Nipashe
No comments:
Post a Comment