Saturday, May 6, 2017

WADAIWA SUGU 300 WAFIKISHWA KORTINI

ZAIDI ya wadaiwa sugu 300 wa kodi ya ardhi katika wilaya mbili za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza wamefikishwa kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba ili walipe.

Miongoni mwa wadaiwa hao ni taasisi za serikali za Mamlaka ya Mapato (TRA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Shirika la Reli (TRL).

Hatua hiyo imetekelezwa na ofisi ya Kamishina wa Ardhi Kanda ya Ziwa, kufuatia agizo la Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Wiliam Lukuvi.

Akiwa ziarani mkoani hapa mwishoni mwa mwaka jana, Lukuvi alimtaka Kamishna kuwachukulia hatua wamiliki wa ardhi walioshindwa kulipia kodi, ikiwemo kusitisha miliki zao na kuuza mali husika.

Akizungumzia suala hilo kwa niaba ya Kamishina wa Ardhi Kanda ya Ziwa, Ofisa Ardhi Mteule (masuala ya kodi ya ardhi), Elia Kamihanda aliwaambia waandishi wa habari kuwa wadaiwa hao wamevunja masharti ya umiliki ardhi.

“Tumeamua kupeleka maombi ya wadaiwa 310, yakiwamo mashirika ya serikali ili mahakama itupatie haki ya kukamata mali zao ambazo zinahamishika na zisizohamishika kwa ajili ya kupiga mnada, " alisema.

Kwa mujibu wa Kamihanda, wadaiwa hao wamelimbikiza jumla ya sh. bilioni 2.2.

Aidha, Kamihanda alisema kazi hiyo ya kwenda mahakamani ilifanyika Aprili, mwaka jana, na wadaiwa sugu 150 walilipa sh. bilioni 7.2.

No comments:

Post a Comment