SHANGWE, nderemo na vifijo vilitanda kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma
kwa takribani dakika 10 wakati Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya
Kikwete alipohudhuria akiwa miongoni mwa wageni huku wabunge wakitaja
mambo tisa kuwa chanzo cha kumshangilia sana kiongozi huyo wa zamani wa
nchi.
Kikwete, maarufu kama JK, aliingia bungeni asubuhi kushuhudia kiapo cha
mkewe, Mama Salima Kikwete, aliyeteuliwa kuwa mbunge na Rais John
Magufuli Machi mosi, mwaka huu.
Katika kikao hicho cha kwanza cha mkutano wa saba wa Bunge la 11, JK
aliingia ukumbini saa 2:50 asubuhi na kutoka saa 3:20 baada ya kile
kilichoonekana kuwa ni kuzidi kwa shangwe zilizokuwa zinaelekezwa kwake
na wabunge waliokuwa chini ya uongozi wa Spika Job Ndugai. Kwa kiasi
kikubwa, hali hiyo ilionekana kuathiri utulivu na ratiba ya kikao hicho.
Udhibiti wa safari za nje unaofanywa na Serikali ya awamu ya tano tangu
iingie madarakani na kuathiri pia ziara za mafunzo za wabunge; ukosefu
wa kupungua kwa posho za vikao na pia madai ya kuingiliwa kwa kazi za
kamati zao ni baadhi ya mambo yaliyotajwa na wabunge kuwa chanzo cha
kushangiliwa sana JK, wakidai kukumbukia “neema” kadhaa wanazoamini kuwa
sasa hawazipati kwa kiwango sawa na enzi za utawala wake wa awamu ya
nne.
Baada ya kutoka ukumbini, JK alitumia dakika takribani tano kupiga picha
na wabunge na watu mbalimbali waliokuwapo kwenye viwanja vya Bunge,
kisha akaongozana na wasaidizi wake kuanza safari ya kutoka nje ya eneo
hilo.
Kabla hajaingia kwenye gari, JK aliombwa kuongea na waandishi wa habari
kuhusu kilichotokea bungeni lakini hakuwa tayari akisema: "Mimi si
mbunge, siwezi kuzungumza hapa (bungeni)."
ILIVYOKUWA BUNGENI
Dalili za kushangiliwa kwa JK zilianza kuonekana mapema alipoingia
ukumbini baada ya baadhi ya wabunge waliomuona kusikika wakisema
'tumekumiss JK' (tumekukumbuka JK).
Baada ya kupigwa kwa wimbo wa taifa na kuapishwa kwa Mama Salma, Spika
Ndugai aliuliza kwa Katibu wa Bunge juu ya kinachofuata katika ratiba na
kujibiwa kuwa ni kipindi cha maswali.
Hapo, Spika akasema kuwa kabla ya kipindi hicho kuanza, atambulishe
kwanza wageni mashuhuri waliopo bungeni na ndipo akamtaja JK na kuamsha
shangwe za wabunge zilizodumu takribani dakika 10.
Spika Ndugai alikiri kuwa haijawahi kutokea mgeni kushangiliwa kiasi
hicho ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria katika kipindi chote cha
ubunge wake.
"Waheshimiwa wabunge, mimi binafsi hiki ni kipindi cha nne nikiwa
bungeni… sijawahi kuona mgeni akipokelewa kwa kiwango hiki," alisema
Ndugai.
Baadhi ya wabunge walisikika wakiomba JK aingizwe kwenye Ukumbi wa Bunge
ili awasalimie huku Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT - Wazalendo), Zitto
Kabwe, akiomba fursa ya kupatiwa nafasi ya kutoa hoja kupitia
'utaratibu' wa Bunge, ambayo hakupatiwa, hata hivyo.
Baada ya kuona Bunge zima linashangilia, Spika Ndugai aliwataka wabunge
kumpa heshima zaidi JK kwa kumshangilia wakiwa wamesimama.
"Kwa makofi hayo, sasa naomba mumpe 'standing ovation' (heshima
wanayoitoa watu waliokuwa wamekaa kwa kusimama na kumshangilia mtu
aliyefanya jambo muhimu)," alisema Ndugai.
WABUNGE WATAJA MAMBO 9
Wakielezea sababu ya kuwapo kwa shangwe hizo ambazo Spika Ndugai alikiri
kuwa hajawahi kuzishuhudia hapo kabla, baadhi ya wabunge walitaja mambo
tisa kwa nyakati tofauti.
Mosi, ni hali ya wabunge kukumbukia baadhi ya mambo wanayoamini kuwa
yalikuwa mazuri enzi za JK lakini sasa hayapo. Mbunge wa Rombo, Joseph
Selasini (Chadema), alisema kitendo cha JK kushangiliwa sana bungeni
ndicho kinachoashiria jambo hilo.
"Haijawahi kutokea ndani ya Bunge mgeni kushangiliwa kiasi hiki.
Hii si mara ya kwanza marais wastaafu kuingia bungeni. Huu ni ujumbe kwa
serikali iliyopo madarakani. Leo (jana) wabunge wamesema kwa vitendo
kwa kumshangilia kupita kiasi rais aliyeondoka madarakani," alisema.
Aliongeza: "Kilichonishangaza kuliko vyote ni aina ya ushangiliaji.
Wabunge wamepiga makofi, lakini pia wamesimama, na waliosimama ni mpaka
Waziri Mkuu na mawaziri wengine.
"Na bado wametamka wazi kuwa wanaisoma namba, na wengine wanamwambia JK kwamba wamemkumbuka.
Ni ujumbe kwa serikali. Inapaswa kujitathimini. Na hawa si watu wa mtaani, ni wabunge,” alisema Selasini.
Pili, zuio la kurushwa moja kwa moja kwa matangazo ya Bunge kupitia
vituo vya luninga. Hii ni sababu iliyotajwa pia na Selasini kuwa
imesababisha wao kumkumbuka zaidi JK na kujihisi kuwa ‘wame-mmiss”.
" Kufunga Bunge 'live' ni tatizo, wabunge wanataka wanachokifanya
bungeni kionekane kwa wananchi wao. Haya ni baadhi ya mambo yaliyofanya
wabunge wamshangilie sana JK.
Aidha, Selasini alitaja jambo la tatu kuwa ni kucheleweshewa malipo yao
na Serikali, jambo ambalo wakati wa JK lilikuwa nadra kutokea.
“Kuna wakati posho na mishahara inachelewa. Kipindi cha JK hatukuwahi kukosa pesa za uendeshaji wa Bunge," alisema Selasini.
Jambo la nne, kwa mujibu wa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT),
ni hisia za kutokuwapo kwa uhuru wa kutosha wa kuzungumza na demokrasia
kulinganisha na ilivyokuwa wakati wa JK.
"Kikwete alitumia muda wake wa uongozi kutoa uhuru kwa watu kusema
watakacho, na hata waliokuwa wanamtukana, yeye alikuwa kama mzazi,
hakuchukua hatua zozote.
Aliachia vyama vya upinzani vifanye siasa bila shida yoyote. Kwa hiyo,
watu wamekumbuka hayo ambayo kwa sasa hayapo. Ndiyo maana
wakamshangilia," alisema Zitto.
Jambo la tano, ni kutofuatwa kwa sheria ya bajeti. Mbunge wa Iringa
Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alidai kusuasua kwa serikali
kutekeleza miradi ya maendeleo ndicho kiini cha JK kushangiliwa kwa
mbwembwe bungeni.
"Serikali inakiuka sheria za nchi. Bajeti haijatekelezwa na kuna pesa
zimetumika bila idhini ya Bunge…hatukuwa na bajeti ya kuhamia Dodoma.
Sheria zinakiukwa waziwazi. Wakuu wa wilaya leo wana ving'ora," alisema
Msigwa.
Jambo la sita, ambalo ni kwa mujibu wa Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein
Bashe (CCM), ni mchango ambao JK aliutoa katika kukuza siasa na
demokrasia nchini, huku akiwataja baadhi ya wanasiasa walionufaika na
hilo kuwa ni pamoja na yeye .
"JK ameshangilia kwa sababu wabunge wengi amewakuza kisiasa. Kina
William Lukuvi (Waziri wa Ardhi, Nyumba naa Maendeleo ya Makazi) na hata
mimi binafsi. Kipindi cha Kikwete ndiyo nilikua kisiasa.
Amewagusa wabunge wengi. Kama alivyosema Nay wa Mitego -- 'waliommiss'
(waliomkumbuka) JK wapo, ndiyo kama wabunge," alisema Bashe.
Jambo la saba, ni udhibiti wa safari za nje. Mbunge wa Ukonga, Mwita
Waitara (Chadema), alidai kuzuiwa kwa safari za nje za wabunge ni sababu
mojawapo ya kushangiliwa sana JK kwa sababi enzi za utawala wake
walipat fursa hizo.
Jambo la nane, ni hisia za baadhi ya wabunge kuwa Serikali ya sasa
imekuwa ikiingulia majukumu ya Bunge mara kwa mara, na hasa kwa
kuingilia utendaji wa kamati zake kiasi cha baadhi ya viongozi (wa
kamati) kuamua kujiweka kando.
"Tumeshuhudia baadhi ya viongozi wa kamati za Bunge wanajiuzulu kutokana
na serikali kuingilia majukumu yao…kitu kama hiki hakikuwahi kutokea
kwenye uongozi wa JK, " alidai Waitara.
Sababu ya tisa, kwa mujibu wa Waitara, ni miradi iliyopitishwa katika bajeti kutotekelezwa ipasavyo.
“Miradi mingi iliyoidhinishwa na Bunge haijatekelezeka, imekwama. Bajeti
imekwama halafu serikali inaongeza bajeti,” alisema na kuongeza:
"Kikwete ameshangiliwa kwa mapenzi ya dhati ya watu… kwamba ni mtu ambaye wanamkumbuka."
SABABU ZAIDI
Mbunge wa Welezo, Saada Mkuya Salum (CCM), alisema JK amepata mapokezi
makubwa bungeni kutokana na mambo mazuri aliyoyafanya katika miaka 10 ya
uongozi wake.
"JK alifanya makubwa sana kwa Tanzania kiuchumi na kuitangaza Tanzania
kimataifa. Aliimarisha miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege.
Watu wanakubali mchango wake katika taifa hili ni mkubwa na ndiyo maana
ukaona wabunge wanamshangilia. Hicho ndicho kiliwatokea wabunge leo
(jana)," alisema.
John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), alisema uhuru wa Bunge umeminywa hivi sasa na ndiyo mana JK alishangiliwa sana.
No comments:
Post a Comment