Wednesday, May 3, 2017

WANAOANDAA HOTUBA YA UPINZANI WAPEWA ONYO NA SPIKA NDUGAI


SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amewaonya vijana wanaoandaa hotuba za Kambi ya Upinzani bungeni, kwamba wawe makini na uandishi wa hotuba za kambi hiyo.

Amesema kwamba, siyo jambo la busara kwa vijana hao kuandika hotuba zinazomtukana Spika wa Bunge wakati ndiye anayewalipa mishahara yao.

Spika Ndugai aliyasema hayo jana mchana wakati alipokuwa akijiandaa kuahirisha Bunge hadi jana jioni.

 “Naomba niseme baadhi ya maneno katika hotuba za upinzani kudharau kiti na kudharau Bunge. Siku moja alisoma hotuba dada yangu hapa Ruth Molel ambaye namfahamu vizuri, kwamba ni mtu ‘Senior’ hata kwangu na ni mtu mwelewa. Nilijua hawezi kuandika yale aliyoyasoma hapa.

“Kwa hiyo, nikafanya utafiti wangu na kugundua kwamba, kwenye ofisi ya upinzani bungeni, kuna vijana wanne ambao ni Onesphori Mbuya, Oliver Mwikila, Jonathan Wilfred na Dorith Konela.

“Vijana hawa waliombewa kazi na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, kwamba wanawahitaji kwa ajili ya kuongeza nguvu kidogo za kufanya utafiti na kusaidiana katika kuandika mambo mbalimbali ikiwamo taarifa wanazosoma.

“Hawa vijana tunawalipa sisi Bunge na kwa maneno mengine, nawalipa mimi, halafu wanakaa wanaandika hotuba za kunituhumu mimi.

“Sijawahi kuona vitu vya namna hiyo na nyinyi mnalijua hili, kwamba siku hizi ajira hakuna. Hivi unamtuhumu mwajiri wako kizembe kizembe tu, uliona wapi duniani kitu kama hicho?

“Kwa hiyo, nawaambia ndugu zangu, niliwahi kusimama hapa na kusema tena na tena, lakini sasa nimechoka na tutaanza kuchukua hatua ingawa hao nao leo nawasamehe kwa sababu hayo ni mambo ya ajabu tena ya kijinga kabisa.

“Pili, wewe unayekuja kusoma hotuba hapa, isome hotuba yako mwenyewe kwa sababu ukija hapa na kuanza kutuhumu Bunge na kumtuhumu Spika ovyo, nitakuvaa wewe mwenyewe, kwamba hayo ni ya maneno yako.

“Hatuwezi kwenda hivyo, mkiifanya taasisi hii kila mtu awe anaropoka anavyotaka, hatutafika popote. Maneno mengine unaweza kuyasema, lakini kama yanahusu taasisi hii, hatuwezi  kuruhusu.

“Nitawalinda kama mlivyosema leo (jana) na kwa wivu mkubwa kwani hii taasisi ni ya kuilinda ili kama mna jambo lolote mliseme kwa sababu kiongozi wenu wa upinzani ni mjumbe wa Kamati ya Uongozi, ni mjumbe wa Kamati ya Kanuni na ni mjumbe wa Tume ya Bunge.

“Katika uongozi wa Bunge hili, nikitoka mimi Spika, anafuata yeye. Kwa hiyo kitendo cha kuja mnasimama hapa na kuanza kututuhumu, maana yake anawatuma yeye kwani yeye ni sehemu ya uongozi.

“Lakini, tukumbuke kwamba, Spika ndiye kama baba yetu, yaani mambo yakikuendea mrama kivyovyote vile, utarudi kwake, ukiugua utarudi hapa, ukifanya nini, utarudi hapa.

“Sasa huyo unayemtukana na kumdharau, naye akichukua roho kama ya kwako itakuwa kama alivyowahi kusema Rais Magufuli pale Zanzibar, kwamba hivi ukiugua mkono wangu unaweza kuidhinisha uende India?, alisema Spika Ndugai.

Kwa mujibu wa Spika, wabunge wanatakiwa kupendana na kuheshimiana kama ambavyo wamekuwa wakifanya kazi pindi wanapokuwa kwenye kamati zao mbalimbali.

No comments:

Post a Comment