Wednesday, May 3, 2017

KUNA MSUVA NA MBARAKA WA KAGERA, LAKINI KOTEI SI MCHEZO


Wakati ikielezwa kuwa kiungo wa Simba, James Kotei, ana asimilia 90 ya kuchukua Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, makocha wengi wamewataja wachezaji wengine.


Kotei ambaye amejiunga na Simba katikati ya msimu huu, amekuwa nguzo sahihi kwenye timu hiyo huku akifanikiwa kuiweka kwenye nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu.

Kwa mujibu chanzo cha ndani kutoka Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao ndiyo hufanya mchakato wa mchezaji bora wa msimu, hadi sasa jina la mchezaji huyo raia wa Ghana ndiyo lipo juu na anaweza kuitwaa.

Kama kiungo huyo mkabaji atashinda basi atakuwa mchezaji wa kwanza kuanzia katikati ya msimu na kuitwaa tuzo hiyo ambayo msimu uliopita alichukua Juma Abdul wa Yanga ambaye msimu huu ameshindwa kuwika.

“Mpaka sasa bodi wanafanya mchakato wa mchezaji bora na kiungo wa Simba James Kotei kama mambo yatamalizika kama yalivyo, yeye ndiye anapewa nafasi kubwa sana ingawa mechi zilizobaki zinaweza kumpindua.

“Watanzania wengi wamekuwa wakifikiria sana tuzo kwenda kwa mshambuliaji, siyo kweli hata ukitazama England kwa sasa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kulipwa (PFA) imekwenda kwa kiungo mkabaji N’golo Kante wa Chelsea,” kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, mchezaji huyo atakuwa amewafunika Yanga ambao msimu uliopita walizoa tuzo nyingi muhimu ambapo pamoja na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora, pia Thaban Kamusoko wa Yanga pia alitwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni huku Kipa wa Azam Aishi Manula akitwaa kipa bora na Amissi Tambwe ufungaji Bora.


Hata hivyo jana makocha mbalimbali wa Ligi Kuu Tanzania Bara waliwataja wachezaji wengine ambao wanaona wanastahili kutwaa tuzo hiyo tofauti na Kotei ambapo Simon Msuva alipata kura moja kati ya makocha sita, huku Mbaraka Yusuf akizoa kura tatu na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye msimu uliopita alichukua tuzo ya Mchezaji Bora Anayechipukia akizoa kura mbili.


Alipoulizwa Kocha wa Mbao FC, Ettiene Ndayiragije, anaona ni mchezaji gani anafaa kutoa tuzo hiyo, alimtaja Msuva wa Yanga, lakini makocha wengine, Seleman Matola aliyewahi kuwa kocha wa Simba, Kocha wa Stand, Athumani Bilal na Mecky Maxime wa Kagera Sugar, walisema kuwa tuzo hiyo apewe Mbaraka Yusuf wa Kagera Sugar.


Makocha wawili ambao walimpa beki wa Simba, Mohammed Hussein Zimbwe au Tshabalala ni Zubery Katwila wa Mtibwa na Hans van Der Pluijm, kocha wa zamani wa Yanga.


Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara atajinyakulia tuzo na kitita cha shilingi milioni 9.2.

No comments:

Post a Comment