Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe
(Mb), jana tarehe 03 Mei, 2017 alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho
ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, jijini Mwanza.
Mhe.
Mwakyembe alipokea hotuba na matamko kutoka kwa Mabalozi na wawakilishi
wa taasisi mbalimbali zikiwemo Umoja wa Mataifa, UNESCO, Umoja wa Nchi
za Ulaya, Baraza la Habari Tanzania, Mfuko wa Vyombo vya Habari na Klabu
za Waandishi wa Habari Mikoani.
Katika
hotuba yake, Mhe. Mwakyembe aliwahakikishia Wanahabari kwamba Serikali
itaendelea kuweka mazingira bora, salama na wezeshi ili kuilea na
kuikuza tasnia ya habari.
Mwakyembe
aliwakumbusha wanahabari kwamba Serikali tayari ilishakamilisha
utungaji wa Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa na Sheria ya Huduma za
Habari ambazo zote zimekamilika mwaka 2016, hivyo wazizingatie katika
utendaji kazi wao.
Mwakyembe
pia aliwasihi wanahabari kuwa wakweli na kuzingatia misingi na maadili
katika kazi zao. "Mlinzi wa kwanza wa Waandishi wa Habari ni Mungu,
Mlinzi wa Pili ni Kalamu ya Mwandishi mwenyewe hasa anapozingatia
maadili ya kazi yake," alisisitiza Mhe. Mwakyembe.
Mhe.
Mwakyembe alielekeza Idara ya Habari ya Habari-Maelezo kuwa na
utaratibu wa kukutana na Wahariri wa Vyombo vya Habari mara kwa mara ili
kubadilishana mawazo na kutoa taarifa sahihi za Serikali.
Aidha,
Mhe. Mwakyembe aliwashauri wanahabari kuzichukulia taarifa za mitandao
ya kijamii kama "tetesi" ambazo huitaji utafiti kabla ya kuzitumia.
Mhe.
Mwakyembe alivitaka vituo vyote vya runinga na redio viwe vinasoma
vichwa vya Habari tu vya magazeti na visisome habari hizo kwa kina mpaka
kurasa za ndani za magazeti kwa kufanya hivyo kunaathiri biashara za
magazeti.
Mhe.
Mwakyembe pia alitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa hakuna uhuru usio na
mipaka hivyo wanahabari watimize wajibu wao bila husda wala mawaa na
kuzingatia misingi ya sheria na taaluma.
Aidha,
Mhe. Mwakyembe aliwaahidi wanahabari wote ushirikiano wa karibu kwa
wakati wote na aliweka utaratibu wa kukutana nao mara kwa mara ili
kutazitatua changamoto zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment