Wednesday, August 9, 2017

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA APOKEA MSAADA WA MAGARI KUTOKA KAMPUNI YA FOTON



Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amepokea msaada wa magari matatu yenye thamani ya Dola za Marekani 99,700 kutoka Kampuni ya Foton International Trade Co. Ltd ya nchini China.

Majaliwa amepokea msaada huo  jana Agosti 9, 2017 jijini Dar es Salaam, ambapo alisema magari hayo yatatumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii nchini. Magari hayo ni Sauvana SUV moja na Tunland Double cabin mbili.

“Nashukuru kwa msaada huu wa magari uliotolewa na Kampuni ya Foton kwa Serikali yetu. Magari haya yanaweza kutumika katika Hospitali za wilaya kwa ajili ya usambazaji wa dawa na vifaa tiba pamoja na kutolea elimu mbalimbali kwa umma.”

Naye, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Zhao Xiao alisema wametoa msaada huo wa magari kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Tanzania hususan maeneo ya vijijini.

Xiao alisema Kampuni ya Foton inatengeneza magari 700,000 kwa mwaka, ambayo  yanauzwa katika nchi 125 duniani. Amesea ifikapo mwaka 2020 wanatarajia kuongeza uzalishaji na kufikia magari milioni 1.4 kwa mwaka.

Kuhusu suala la kuja kuwekeza kwenye ujenzi wa kiwanda cha kuunganisha magari nchini, Bw. Xiao alisema wanampango wa kuwekeza nchini kwa kuwa  kuna fursa nzuri za uwekezaji na uhakika wa masoko katika nchi zingine za Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment