Tuesday, February 20, 2018

WAZIRI KINGWANGALLA AITEMBELEA FAMILIYA YA AKWILINA NA KUTOA UBANI WA POLE


Mbunge wa Jimbo la Nzega Vijijini ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla jana ali tembelea nyumbani kwa familia ya Akwilina na kutoa ubani wa pole kwa msiba huo.

“Nimefika hapa kama Raia mwema tu ambaye nimeguswa na msiba huu na nimetafakari kwani na mimi kipindi fulani nilipitia chuo hasa kutoka familia zetu hizi masikini kwa hiyo inapotokea tukio kama ili unaona ni pigo kwa familia, pigo kwa jamii, pigo kwa wanafunzi wenzake na pigo kwa Taifa kwa ujumla wake” alieleza Dkt. Kigwangalla wakati akizungumza na vyombo vya Habari msibani hapo.

“Ndoto za binti huyu zimezimika ghafla, nimesikitika sana, nimekuja kujumuika na Watanzania wenzangu kumlilia Akwilina, nmeguswa na msiba tuendelee kumlilia ....sidhani kama ni wakati muafaka kuanza kunyoosheana vidole nani kafanya nini, hili halina umuhimu kwa sasa,”  Aliongeza Kigwangalla

Dkt.Kigwanalla ambaye alifika msibani hapo majira ya saa saba mchana, aliweza kuungana pamoja na ndugu na jamaa wa wafiwa ambapo pia alipata chakula cha mchana pamoja na waombolezaji wengine sambamba na kutoa ubani wake kama mwananchi mwingine.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makoli ambaye yupo hapo kwa ajili ya kusimamia shughuli  kwa upande wa Serikali, alibainisha kuwa wataendelea kuratibu baadhi ya mambo yanayoendelea hapo kwani msiba huo kwa namna moja Serikali imeguswa nao.

Mbali na Mkuu wa Wilaya hiyo, Wengine waliofika hapo ni pamoja na Mkurugenzi wa Ubungo, John Kayombo ambapo kwa pamoja na watendaji wengine wa Kiserikali wameweza kusaidiana na familia ya marehemu katika shughuli mbalimbali zinazoendelea msibani hapo.

Akwilina kabla ya kifo chake alikuwa Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji(NIT) amepoteza maisha baada ya kupigwa risasi Februari 16 mwaka huu eneo la Mkwajuni jijini Dar es Salaam wakati Polisi walipokuwa wakizuia maandamano ya chama cha siasa cha CHADEMA.

No comments:

Post a Comment