SAKATA la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuvamia kituo cha televisheni
cha Clouds liliibuliwa upya na wadau wa habari jana baada ya kulilaani.
Wadau hao wa habari walilaani tukio hilo jana ikiwa ni siku maalum ya Uhuru wa Habari iadhimishwayo Mei 3 kila mwaka.
Akizungumza kama mgeni rasmi katika siku hiyo jijini, Mbunge wa viti
maalum wa Chama Cha Wananchi (CUF), mkoa wa Dar es Salaam, Salma Mwasa
alisema si jambo jema viongozi wa umma kuonekana wanakuwa mstari wa
mbele kuminya uhuru wa habari.
Alisema kitendo alichokifanya mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam ni cha
kulaaniwa na kitaendelea kulaaniwa na kila mpenda amani na mpenda ustawi
wa vyombo vya habari, na anayetambua umuhimu wake katika nchi.
“Viongozi wa umma na watunga sera, wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika
kulinda vyombo hivi vya habari na kuhakikisha vinafanya kazi yao kwa
uhuru," alisema Mwasa.
"(Viongozi wa umma) wanapogeuka na kuonyesha wa kwanza kuviminya (vyombo
vya habari) inaonyesha sifa mbaya na hawapeleki ujumbe mzuri kwa hawa
wengine wanaowategemea, wanaowasikiliza na kuwaamini.
“Kiukweli kile kitendo kinatakiwa kulaaniwa na kitaendelea kulaaniwa,
kwa sababu pasipo kufanya hivi, vitendo hivi vinaweza kuendelea
kufanyika na huko tunakoenda hali ya uhuru wa vyombo hivyo inaweza ukawa
mgumu zaidi.”
Tukio hilo la staili ya utekaji wa vituo vya habari wakati wa mapinduzi
ya kijeshi, lilifanywa na mkuu huyo Machi 17 saa 5 usiku.
Mkuu huyo alionekana katika video zilizosambaa kwenye mitandao ya
kijamii akiwa na askari wasielekea kuwa polisi, waliokuwa na bunduki.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamati ya waziri iliyochunguza sakata hilo,
mkuu huyo alivamia kituo hicho usiku huku vipindi vikiwa vinaendelea na
kwamba aliwatisha na kuwalazimisha watangazaji wa kipindi cha Shilawadu
kuonyesha taarifa yake.
Taarifa hiyo ya upande mmoja, ilikuwa ikimtuhumu Askofu wa Kanisa la
Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuwa amezaa na muumini wake.
Gwajima ambaye alikanusha vikali madai hayo kanisani kwake, alianzisha
tuhuma za mkuu huyo kutumia cheti feki kujiunga na elimu ya juu na
kwamba jina lake halisi ni Daud Bashite.
Mwasa alisema hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini inazidi kuwa
mbaya kadri siku zinavyosonga na kwamba licha ya changamoto wanazokutana
nazo, waandishi wa habari hawapaswi kukata tamaa.
“Tumeshuhudia baadhi ya waandishi wanapigwa na wengine hata kujeruhiwa
wanapokuwa wanafanya kazi zao," alisema Mwasa. "Nataka kuwaomba wasikate
tamaa."
"Watanzania wanawategemea, wakumbuke kuwa hakuna ukombozi bila mateso,
tunajua wako katika wakati mgumu lakini tunaomba hali hiyo isiwakatishe
tamaa.”
Alisema wao kama wawakilishi wa wananchi, wataendelea kupambana
kuhakikisha uhuru huo unalindwa hata ikiwezekana kujenga hoja bungeni
ili Sheria ya Vyombo vya Habari iliyopitishwa hivi karibuni irudishwe
bungeni ili baadhi ya vipengele ambavyo vilionekana kuwa vina mtego kwa
waandishi hao, virekebishwe.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za
Siasa (Taporea), George Maziku alisema ripoti ya hali ya uhuru wa
waandishi wa habari iliyotolewa na Shirika la Waandishi wa Habari Wasio
na Mipaka inaonyesha kuwa katika miaka 10 iliyopita zaidi ya waandishi
800 kutoka mataifa mbalimbali duniani wameuawa wakiwa wanatekeleza
majukumu yao.
Akizungumzia Sakata la Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kuvamia kituo cha
televisheni, alisema ni jambo la kusikitisha kuona mpaka sasa hakuna
hatua yoyote ambayo mkuu huyo amechukuliwa.
No comments:
Post a Comment