Thursday, May 4, 2017

MBUNGE AMWAGA CHOZI BUNGENI AKIZUNGUMZIA UDHALILISHAJI WA WATOTO


Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Faida Bakari amemwaga chozi bungeni akielezea udhalilishaji unaofanywa kwa watoto nchini.

Faida akichangia bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha 2017/18 bungeni jana mjini Dodoma alisema watoto wanadhalilishwa kwa kufanyiwa vitendo vibaya na watu wazima. Aliiomba Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wanaobainika kufanya hivyo.

“Watoto wanaharibiwa mheshimiwa waziri, naomba mchukue hatua kali za kisheria kwa watu hawa. Nilienda Pemba nililia watoto wanaharibiwa maumbo. Mheshimiwa nasema kwa uchungu,” alisema huku akilia na kuvuta pumzi ndefu kabla ya kuendelea kuzungumza.

Alisema walimu wamekuwa wakiwadhalilisha watoto huko Pemba na kumuomba waziri ashughulikie suala hilo.

“Tumrudie Mungu, unakuta mibaba mizima inawapa mimba watoto na madevu yao mengi wanawatia watoto wenzao mimba,” alisema.

Faida pia alisema wazee wamekuwa wakinyanyaswa katika jamii na kuwataka Watanzania kuwatunza kwa sababu ipo siku nao watakuwa wazee. “Ukiona nyumba zao unalia naomba  mheshimiwa uangalie katika eneo hili la wazee.”

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo yeye alisema wazee wametelekezwa katika kambi za kuwahudumia na kuitaka Serikali kuwaangalia.

“Mwaka jana mlisema mtaleta Sheria ya Wazee lakini mwaka huu haikuzungumzwa, hakuna sheria ya wazazi ndiyo maana wazee bado wanauawa,” alisema.

No comments:

Post a Comment