Makongoro Mahanga
Dar es Salaam. Kamati ya Maandalizi ya kongamano lililoandaliwa na Chadema imesema serikali ya mkoa wa Dar es Salaam imewazuia kutumia ukumbi wa Anatouglou waliouomba kwa ajili ya kongamano hilo.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Makongoro Mahanga imeeleza kuwa wamepewa taarifa ya ghafla na serikali ya mkoa ya kuwazuia kufanya kongamano hilo leo Mei 13.
“Hata hivyo kwa mshangao mkubwa, usiku huu tumepata taarifa kwamba Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam imezuia matumizi ya ukumbi huo kwa ajili ya kongamano hilo kwa kile tulichoambiwa ni kujitokeza kwa shughuli nyingine za Mkoa kwenye Ukumbi huo hiyo kesho,” imesema taarifa hiyo na kuongeza:
“Kutokana na hali hiyo na muda uliopo, tunalazimika kuahirisha kongamano hilo hadi litakapotangazwa tena. Tunaahidi kutoa taarifa kamili ya jambo hili kwa vyombo vya habari mapema iwezekanavyo.”
Kadhalika taarifa hiyo imesema kuwa mwaliko wa kongamano hilo ulipelekwa pia kwa viongozi wakuu wa Vyama vyote vikubwa vya siasa nchini vikiwemo CCM, CHADEMA, CUF, NCCR Mageuzi, ACT Wazalendo na CHAUMMA.
No comments:
Post a Comment