MSHAURI wa Chama cha ACT Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo, ametangaza
kuachana na siasa na kuwa mtumishi wa umma kwa asilimia 100.
PROFESA KITILA MKUMBO.
Jana Rais John Magufuli, alitangaza kufanya mabadiliko madogo katika
safu ya Makatibu wakuu na kumteua Profesa Mkumbo kushika nafasi
iliyoachwa wazi na Mhandisi Mbogo Mfutakamba, aliyekuwa Katibu Mkuu wa
wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Profesa Mkumbo alishukuru kwa
uteuzi huo na kueleza kuwa unapopewa kazi na Mkuu wa nchi kinachopaswa
ni kuwajibika kwa niaba yake.
“Nimeipokea kuwa ukipewa kazi na Mkuu wa nchi unaheshimu kazi,
unaheshimu aliyekua kazi yake, unaifanya kwa bidii kadri Mungu
alivyokujalia, name nitafanya hivyo,” alisema na kuongeza:
“Mimi ni mtumishi wa umma, kiutumishi rais ana mamlaka ya kuwatumia kwa
kadri anavyoona, nadhani ameona nitaweza kutumikia kwenye nafasi hiyo,
namshukuru Rais, Namshukuru Mungu, basi nakwenda kuitumikia,” alisema.
Kuacha siasa kwa asilimia 100
Mkumbo alipoulizwa juu ya kuwa na ‘damu’ ya siasa, alisema kuanzia sasa
anasimamisha shughuli za kisiasa na kuwa mtumishi wa umma kwa asilimia
100.
“Mambo ya kisiasa kwa sasa itabidi yasimame, nimsaidie Mheshimiwa rais
kuhakikisha nchi hii inapata maji kama anavyotarajia na sera za
serikali zilivyo,” alifafanua.
Aprili 17, mwaka jana, Mkumbo alikaririwa na vyombo vya habari kuwa “Huu
utaratibu wa kuwateua wasomi tu ambao ni walimu na wanataaluma kutoka
vyuo vikuu hasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) si mzuri maana rais
haoneshi kuwaandaa wengine kuchukua nafasi zao, tuachwe wasomi tufanye
kazi za kitafiti na kitaaluma.”
Alipoulizwa juu ya kuikosoa serikali alisema “Hoja yangu kubwa ilikuwa
ni kwamba serikali inapoteuwa ni lazima iajiri, lazima kuwe na
‘replacement’.”
Kitila ambaye amewahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa,
alipoulizwa tafsiri ya uteuzi huo kwa upinzani, alisema “ni heshima
kwamba mtu mmoja ambaye alikuwa mpinzani anateuliwa maana yake kuna
wapinzani wenye sifa za kiutumishi.”
“Pia ni kumshukuru rais kuwa ana uwezo wa kuvuka mipaka, amevunja ile
miiko kwamba ni lazima utoke chama flani. Mtu kama mimi amenipa mtihani
lazima nikaishi kama mtumishi wa umma kama ambavyo taratibu na sheria
zinazopaswa kuwa,” alibainisha.
Atakalosimamia
Alisema maji ndilo hitaji namba moja la Watanzania na kwamba atafanya
kazi kwa bidii kuhakikisha wananchi wanapata maji kama inavyotakiwa.
Katika kundi la Whatsapp la ACT Habari, wanachama walihoji uongozi wa
ACT jinsi walivyopokea uteuzi huo na kama Profesa Kitila ameupokea.
Afisa habari wa ACT wazalendo, Abdallah Khamisi, aliulizwa wameupokeaje uteuzi wa Profesa, alijibu “vuteni subira”
Zitto:Jambo zito
Aidha, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, katika group hilo,
waandishi walitaka kusikia kauli yao (ACT), lakini akawataka watulie na
alipoelezwa kuwa uchapishaji wa gazeti unakwenda na muda (deadline).
Alisema “Kwa hiyo tufanye mambo yetu kwa deadline yako (kataja jina la mwandishi)? Hili jambo zito sana.”
Septemba 03, mwaka jana, Rais Magufuli akizungumza na Wananchi wa
Zanzibar, alisema “Rais uchaguliwe upate asilimia 92 bado unachukua watu
wa vyama vingine unawaingiza kwenye serikali yako. Mimi nilipata
asilimia 58, hakuna wa chama kingine mle ndani, na wala hataingia,”
Huku akishangiliwa na wana CCM waliohudhuria mkutano huo, alisisitiza
kuwa Dk. Shein ana moyo wa tofauti “amepata asilimia 92 bado analeta
wengine, mimi nimepata asilimia 58 hakuna atakayekanyaga mguu kwenye
serikali yangu.Unguja Hoyee!Zanzibar Hoyee! Ndiyo maana nasema mzee huyu
ana moyo wa tofauti…naomba Mungu anisaidie angalau nipate karobo ka
moyo wako.”
Mnyika: Imedhihirisha alikuwa mamluki
Mjumbe wa kamati Kuu ya Chadema, John Mnyika, alisema uteuzi wa Profesa
Kitila kuwa sehemu ya serikali unadhirisha ilikuwa sahihi kufukuzwa
Chadema.
“Huo uteuzi umedhihirisha maamuzi yaliyofanywa na kamati Kuu ya Chadema
ya kumfukuza uanachama kutokana na usaliti yalikuwa ni sahihi, kwamba
alikuwa anatumika na utawala,” alibainisha Mnyika.
Mwaka 2013, Profesa Kitila, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto na Samson
Mwigamba, walifukuzwa Chadema kwa madai ya kukiuka Katiba, sheria na
kanuni za chama hicho.
Katika uteuzi huo, Rais amemteua Dk. Ave Maria Semakafu kuwa Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, akijaza nafasi
iliyoachwa wazi na Dk. Leonard Akwilipo, ambaye ameteuliwa kuwa Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo.
Kwa alipoulizwa na Nipashe, Dk. Semakafu ambaye ni Mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), alisema hawezi
kuzungumza lolote kwa kuwa bado hajapokea taarifa rasmi zaidi ya kusoma
kwenye mitandao ya kijamii.
“Unajua iko kwenye mitandao mimi sina taarifa, ‘I can not comment
anything’ mpaka nitakapoelezwa ni kitu gani, kila mtu ananipa hongera
ila sijaelewa, naomba msubiri nipate taarifa kamili,” alisema Dk.
Semakafu ambaye pia ni mwanaharakati na Mjumbe wa Bunge Maalum la
Katiba.
Katika uteuzi huo wengine ni Dk. Akwilipo ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na aliyekuwa Katibu Mkuu,
Maimuna Tarishi, amehamishwa na kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
(Bunge).
Kiongozi huyo anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mussa Uledi ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
ZITTO ATOA NENO
CHAMA cha ACT Wazalendo, kimepokea kwa mikono miwili uteuzi wa Prof.
Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji na kwamba
kimekubali barua ya kujiuzulu kwake kwenye nafasi ya ushauri wa chama.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Kiongozi wa Chama hicho
ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe alisema uteuzi huo
umeonesha kuwa Rais Dk. John Magufuli ameona kuwa hata watanzania walio
kwenye Vyama vya Upinzani wana uwezo, weledi na uzalendo wa kutumikia
nchi.
“Kwa hatua hii, tunaona Rais ameamua kuunganisha nchi yetu kwa kufanya
kazi na watu wote bila kuwabagua kwa itikadi zao za vyama. Watanzania ni
wamoja na kauli za kuwagawa zinaumiza zaidi Taifa kuliko kuliweka
pamoja. Tunaamini kuwa Rais Ana nia njema katika uteuzi huu na sisi
tumempa baraka zote Mwanachama wetu na mwanzilishi wa Chama kwenda
kwenye nafasi ya juu zaidi ya utumishi wa umma,”alisema
Alieleza anaamini hatamwangusha Rais na muhimu zaidi hatawaangusha
watanzania na aitumikie nafasi hiyo kwa uadilifu, uaminifu na weledi.
Alisema kutokana na uteuzi huo Prof. Mkumbo hawezi kuendelea kuwa
Mshauri wa Chama nafasi ambayo ilimfanya kuhudhuria vikao vyote vya
Chama ikiwemo Kamati Kuu.
“Ndugu Mkumbo ameandika barua ya kujiuzulu nafasi yake ya mshauri wa
Chama na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida tu. Nimeipokea barua yake na
kumkubalia Kwa maslahi mapana ya nchi yetu,”alisema Mbunge huyo
Alisema ni vigumu Prof.Mkumbo kukataa uteuzi kwa kuwa yeye ni mtumishi
wa umma na hatua hiyo ni kama kupanda cheo kwenye utumishi.
“Prof. Mkumbo tunamshukuru kwa mchango wake katika uongozi wa Chama
chetu kwa wakati wote ambao alikitumikia Chama chetu kama mshauri wa
chama. Msimamo wa chama chetu ni utumishi wa kizalendo kwa Taifa
utokanao na kila mwananchi,”alisema
Alisema Wizara hiyo ni kubwa na muhimu sana kwa nchi kwa kuwa Maji ni
tatizo moja kubwa ambalo wananchi wanakumbana nalo na kama Taifa
halijaweza kulimaliza.
Alibainisha Katibu huyo mteule ataenda kuongeza nguvu ya kumaliza kero
ya maji na kuhakikisha anaimarisha kilimo cha umwagiliaji nchi nzima na
kumtaka aanze na ajenda ya Mfuko wa Maji Vijijini na kuanzishwa Kwa
Wakala wa Maji Vijijini utakaosimamia upatikanaji wa maji kwa wananchi.
Alipoulizwa kama uteuzi huo utakidhoofisha Chama hicho, Kabwe alisema
watu wamekuwa na tafsiri nyingi kuhusu uteuzi huo wengine wakidai
utadhoofisha chama au kufutwa machozi na kwamba chama hakiwezi kulinyima
Taifa mtu mwenye uwezo na weledi.
“Tulichojiuliza tunalinden chama au tulinde nchi tukaona hatuwezi
kuwanyima watanzania mtu kama Kitila aende kuwatumikia,”alisema Kiongozi
huyo
No comments:
Post a Comment