Katibu wa baraza la wazee wa Yanga Mzee Ibrahim Akilimali amesema, huenda kujiuzulu kwa mwenyekiti wa klabu hiyo Yusuf Manji ni kutikisa kibiriti tu lakini atarejea tena kwenye nafasi yake kwa sababu tayari alishawahi kutangaza kujiuzulu halafu akarejea baada ya kuombwa na wanachama kufanya hivyo.
Mzee Akilimali amesema mara ya kwanza Manji alipotangaza kujiuzulu alitukanwa na kutishiwa maisha hadi kutaka kuchomewa nyumba yake lakini baadae Manji alirejea kwa hiyo bado haamini kama amejiuzulu jumla au anatikisa kiberiti kama mwanzo.
“Mimi siamini kwa sababu mguu uliomumwa na nyoka ukikanyaga jani unaogopa, aliposema anajiuzulu basi nilitishiwa amani kabisa na kutukanwa matusi ya laana siwezi kuzungumza nikawa naishi kwa kibali cha polisi ili kunipa usalama lakini alikuwa anatishia, pengine na wakati huu anatishia,” amesema Akilimali wakati akihojiwa na kituo cha EFM Radio.
“Wana Yanga wawe wavumilivu wawe na utulivu kwa sababu hatima tutaisikia kwa sababu mimi nashindwa kuamini, kuna wakati kiongozi wetu alitikisa kibiriti iliniletea mimi kutaka kuawa na kuchomewa nyumba moto lakini kumbe alikuwa anatikisa tu kiberiti mkubwa wetu.”
“Alichokifanya ni haki yake kisheria kwa sababu nimesikia ana matatizo ya kiafya kwa hiyo tumepokea kwa huzuni kwakweli. Kama itathibitika afya yake sio nzuri tutabariki maamuzi yake lakini kama afya yake itakuwa inanafuu tutajaribu kuomba aendelee kidogo kwa sababu wakati mgu huu bado tunamuhitaji.”
Mwezi August 2916 Manji alitangaza kujiuzulu nafasi yake kama mwenyekiti wa Yanga huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni baadhi ya watu kupinga juhudi zake za kujaribu kuikodi nembo ya klabu hiyo kwa miaka 10. Mzee Akilimali ni miongoni mwa watu waliokuwa wakitajwa kupinga utaratibu wa Manji kuikodi Yanga.
No comments:
Post a Comment