WASHAMBULIAJI wote tegemeo wa Yanga, Mrundi Amissi Joselyn Tambwe na
Mzimbabwe Donald Dombo Ngoma hawatasafiri na timu kesho kwenda Zambia
kwa mchezo wa marudiano na wenyeji, Zanaco hatua ya 32 Bora Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Tambwe hakucheza kabisa mechi ya kwanza dhidi ya Zanaco Jumamosi ya
Machi 11, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Ngoma alijitonesha goti
katika mchezo huo baada ya kurejea kufuatia kuwa nje tangu Janauri.
Katibu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema leo mjini Dar es Salaam
kwamba pamoja na wawili hao ambao ni majeruhi, pia klabu itawakosa kipa
Beno Kakolanya, beki Pato Ngonyani, kiungo Yussuf Mhilu na
washambuliaji wengine wawili, wote wazawa, Malimi Busungu na Matheo
Anthony ambao pia ni wagonjwa.
Donald Ngoma akiugulia maumivu baada ya kujitonesha goti katika mchezo wa kwanza dhidi ya Zanaco Jumamosi
Mkwasa amesema wachezaji 20 tu ndiyo watasafari na timu kesho kwa ndege
ya Shirika la Kenya kwenda Lusaka kwa ajili ya mchezo huo wa Jumamosi na
kwa bahati mbaya hakutakuwa na mshambuliaji halisi hata mmoja.
Hao ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’,
mabeki ni Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Hassan Kessy, Juma Abdul,
Vincent Bossou, Andrew Vincent ‘Dante’, Kevin Yondan na Nahodha Nadir
Haroub ‘Cannavaro’.
Viungo ni Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Justine Zulu,
Said Juma ‘Makapu’, Juma Mahadhi, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya,
Obrey Chirwa na Emanuel Martin.
Yanga inahitaji ushindi wa ugenini Jumamosi ili kwenda hatua ya makundi
ya Ligi ya Mabingwa baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 Jumamosi iliyopita
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment