Thursday, March 16, 2017

MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM PAUL MAKONDA AJITETEA KUHUSU WEMA SEPETU

HATIMAYE Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametoa ufafanuzi kuhusiana na sababu za kuwatangaza hadharani watu waliohusishwa na dawa za kulevya wakiwamo Askofu Josephat Gwajima na mshindi wa taji la mrembo wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu.

Akizungumza katika hafla ya kutimiza mwaka mmoja tangu ateuliwe na Rais Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa huo kwenye viwanja vya Oysterbay jana, Makonda alisema uwazi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni miongoni mwa sababu hizo, nyingine zikiwa ni kujiweka kwake mbali na vishawishi vya rushwa na pia kuwadhihirishia wananchi kuwa taarifa wanazotoa kuhusiana na vita hiyo zimekuwa zikifanyiwa kazi bila kusita.

Gwajima ambaye ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo jijini Dar es Salaam, pamoja na Wema ambaye pia ni msanii wa filamu, ni miongoni mwa watu maarufu kadhaa waliotajwa na Makonda katika orodha ya awali ya watuhumiwa 65 wa dawa za kulevya.

Wengine katika orodha hiyo ni pamoja na wanasiasa aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Iddi Azzan; baadhi ya wamiliki wa hoteli na klabu za usiku na pia wasanii wakiwamo Khalid Mohamed ‘TID’ na Chid Benz.

Watuhumiwa hao walitakiwa na Makonda kujisalimisha katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam kwa mahojiano kabla ya hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa kwa baadhi yao.

No comments:

Post a Comment