Yanga walianza harakati za kumsajili Djako ili kumuongeza kikosini katika mechi za hatua ya makundi za Kombe la Shirikisho baada ya straika huyo kucheza vizuri dhidi yao lakini kumbe walishachelewa.
Djako aliinyanyasa Yanga katika mchezo wa marudiano wa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, lakini Championi Jumatano limeambiwa kwamba mchezaji huyo anayelipwa zaidi ya Sh 5 milioni na Dicha akili yake iko Misri.
Mmoja wa wasimamizi wa Djako ambaye pia ni mchambuzi wa nchini Ethiopia, Omna Gebru, amethibitisha kwamba Djako amemalizana na El Entag El Harby mwezi mmoja kabla ya kukutana na Yanga lakini hajawaambia ukweli.
“Arafat Djako huyu wa Wolaitta Dicha atajiunga na El Entag El Harby ya Misri kwa sababu tayari ameshazungumza nao na amekubali kwenda huko kusaini mkataba ule wa awali baada ya kutoka hapa Ethiopia.
“Kwa suala hili sasa linakatisha lengo la Yanga kuipata saini yake kwani nao walikuwa wanamtaka tangu baada ya kumuona wanacheza naye kwenye michezo ile ya mtoano kufuzu makundi.
“Hata nahodha wao (Nadir Haroub ‘Cannavaro’) alisema viongozi wao wamsaini kwa sababu ya uwezo wake,” alisema Gebru.
Djako ndiye mfungaji wa bao pekee na la ushindi la Dicha dhidi ya Yanga katika mechi ya marudiano nchini Ethiopia. Hata hivyo, Yanga ilisonga mbele kwa mabao 2-1 kwani awali ilishinda mabao 2-0.
No comments:
Post a Comment