Thursday, March 16, 2017

YANGA, AZAM: TUTAUA


Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kimataifa, Yanga na Azam FC zote kwa pamoja zimejinasibu kwenda kuwashangaza wapinzani wao kwa kushinda ugenini katika mechi zao za marudiano zitakazochezwa mwishoni mwa wiki hii

Wakati Azam wameondoka jana na kikosi cha wachezaji 23 kwenda Swaziland kurudiana na Mbabane Swallows, Yanga yenyewe inaondoka leo mchana kuelekea Zambia kuumana na Zanaco.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, alisema wanaondoka wakiwa na matumaini ya kufanya vizuri.

"Taarifa nilizonazo tutamkosa Ngoma (Donald) na hatutaondoka naye, huu ni mpira na lolote linaweza kutokea..., tunaenda kupambana kwa lengo la kupata ushindi hiyo ndiyo dhamira ya safari yetu," alisema Mkwasa.

Alisema mshambuliaji mwingine wa timu hiyo, Amissi Tambwe yupo katika hali nzuri baada ya kupona majeraha yake.

Yanga inahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao 2-2 ili kuweza kufuzu kwa hatua inayofuata ya michuano hiyo kufuatia sare ya bao 1-1 waliyoipata kwenye mchezo uliochezwa Jumamosi iliyopita jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wao Azam, Ofisa habari wa timu hiyo, Jaffar Iddi, aliiambia Nipashe jana muda mfupi kabla ya kuondoka kuwa kikosi cha timu hiyo chenye wachezaji 23 kimeenda Swaziland kumalizia kazi waliyoianza wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Jaffar, alisema kikosi cha timu hiyo kimeondoka kikifahamu kina kazi kubwa mbele yake kutokana na ubora wa wapinzani wao.

"Benchi la ufundi la Azam linafahamu kabisa kuwa kazi bado haijaisha, tutacheza kwa nidhamu ya hali ya juu na kutokana na uzoefu wa wachezaji wetu tuna uhakika wa kufanya vizuri," alisema Jaffar.

Timu hiyo imeongozwa na mwenyekiti wake Idrisa Nassor pamoja na Meneja wao Mkuu, Abdul Mohamed huku mkuu wa msafara huo akiwa ni mjumbe kutoka Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Azam inahitaji ushindi au sare yoyote ili kuweza kusonga mbele.

No comments:

Post a Comment