VIGOGO Simba SC wanateremka kwenye Uwanja wa Maji Maji mjini Songea kumenyana na wenyeji Maji Maji katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Simba wataingia kwenye mchezo wa leo wakiwa na kumbukumbu ya kucheza mechi mfululizo za Ligi Kuu bila kushinda, wakitoka kulazimishwa sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro na kufungwa 1-0 na Azam FC, Dar es Salaam.
Kwa Maji Maji hali ndiyo mbaya zaidi, kwani wamecheza mechi tano mfululizo bila kushinda tangu walipoifunga Mwadui 1-0 Jumapili ya Novemba 6, mwaka jana Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.
Desemba 18 walifungwa 1-0 na Tanzania Prisons mjini Mbeya, Desemba 24 walilazimishwa sare ya 1-1 na Azam FC Songea, Desemba 28 walifungwa 1-0 na Mtibwa Sugar, Januari 17 walifungwa 1-0 na Yanga Songea na Januari 28 walilazimisha sare ya 0-0 na Ndanda Mtwara.
Kwa sababu hiyo, mchezo wa leo unatarajiwa kuwa mgumu kutokana na kila timu kuingia uwanjani kupigania ushindi.
Kwa sasa Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zao 45 baada ya kucheza mechi 20, nyuma mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 46 za mechi 20.
Wakati Simba inapigania ubingwa, Maji Maji yenyewe inapambana kuepuka kushuka daraja, hadi sasa ikiwa inashika nafasi ya 15 kwa pointi zake 18 za mechi 20, kwenye Ligi ya timu 16. Inaizidi pointi mbili tu JKT Ruvu inayoshika mkia.
No comments:
Post a Comment