Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo
tarehe 08 Februari, 2017 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 6
kutoka nchi mbalimbali walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi
wote wana makazi yao hapa Jijini Dar es Salaam na wamekabidhi hati zao
za utambulisho kwa Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mabalozi
hao ni Balozi wa Ufalme wa Kiarabu wa Saudi Arabia Mhe. Mohamed Ben
Mansour Al Malek, Balozi wa Ufalme wa Morocco Mhe. Abdelilah Benryane,
Balozi wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Benson Keith Chali, Balozi wa Jamhuri
ya Cuba Mhe. Lucas Domingo Hernandez Polledo, Balozi wa Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran Mhe. Mousa Farhang na Balozi wa Jamhuri ya Burundi Mhe.
Gervais Abayeho.
Pamoja
na kupokea hati zao za utambulisho Mhe. Rais Magufuli amewakaribisha
Mabalozi hao hapa nchini na kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea
kushirikiana na nchi zao katika nyanja mbalimbali hasa uchumi kwa
manufaa ya pande zote.
“Mhe.
Balozi najua kuwa Saudi Arabia imekuwa ikishirikiana na Tanzania
kutekeleza miradi mingi ya ujenzi wa miundombinu na bado kuna miradi
mingi tutashirikiana, naomba umfikishie salamu zangu nyingi Mhe. Mfalme
wa Saudi Arabia kuwa tutaendelea kushirikiana” amesema Mhe. Rais
Magufuli alipokuwa akizungumza na Mhe. Balozi Mohamed Ben Mansour Al
Malek.
“Nitafurahi
sana kuona Cuba inakuja kujenga viwanda vingi vya kuzalisha dawa hapa
Tanzania, tunataka kuondokana na uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi ili
kupunguza gharama kubwa ambazo Serikali inabeba kwa sasa kwa kuagiza
dawa kutoka nje” Mhe. Rais Magufuli amemueleza Balozi wa Cuba hapa
nchini Mhe. Lucas Domingo Hernandez Polledo.
Balozi
wa Morocco hapa nchini Mhe. Abdelilah Benryane amemueleza Rais Magufuli
kuwa pamoja na mambo mengine ambayo nchi hiyo inaendelea kushirikiana
na Tanzania tayari imeanza mchakato wa kutekeleza ahadi ya Mfalme wa
Morocco Mtukufu Mohammed VI ya kujenga uwanja wa mpira Mjini Dodoma.
Akizungumza
na Balozi wa Zambia hapa nchini Mhe. Benson Keith Chali Mhe. Rais
Magufuli amesema anatarajia ujio wake pamoja na mambo mengine utasaidia
kuharakisha mchakato wa kuimarisha utendaji kazi na ufanisi wa reli ya
TAZARA na bomba la mafuta la TAZAMA kwa manufaa ya nchi hizi mbili.
Kwa
Balozi wa Burundi hapa nchini Mhe. Gervais Abayeho, Mhe. Rais Magufuli
amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi hiyo kama
ndugu na marafiki wa kihistoria na kwamba anaamini kuwa juhudi
zinazoendelea kufanywa na Mpatanishi wa Mgogoro wa kisiasa nchini humo
Mhe. Benjamin William Mkapa ambaye ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu
nchini Tanzania zitazaa matunda.
Mabalozi
wote wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa hatua anazochukua kujenga
uchumi wa Tanzania, kukabiliana na rushwa, matumizi mabaya ya madaraka
na kusimamia uwajibikaji wa viongozi na watumishi wa umma.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es saalam
No comments:
Post a Comment