Tuesday, June 12, 2018

WAZIRI ATOA AGIZO KUHUSU BEI ZA MAJI NCHINI

Waziri  wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe, ameagiza ifikapo Julai Mosi mwaka huu, Mamlaka za maji nchini zihakikishe zinabadilisha bei ya maji ili ziweze kujitegemea kimapato.

Kamwelwe alitoa kauli hiyo jijini hapa jana alipokuwa akifungua kikao cha kazi cha wadau wa sekta ya maji nchini.

“Tumebakiza siku 20 au 19 tufike tarehe moja Julai, nishukuru Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) wapo hapa, hii kelele za bill (ankra) ya maji, bill (ankra) za umeme Tanesco wanatukatia umeme baada ya moja Julai nawaeleza kila mamlaka ya maji ibadilishe tariff ili iweze kujitegemea,” aliagiza.

Alisema kwa kuwa Mkurungezi wa Ewura alikuwa kwenye kikao hicho na amesikia maelekezo hayo kama atasema wamekata umeme kwenye miradi ya maji au wameshindwa kununua dawa za kutibu maji, atakuwa hatoshi.

“Mi nimenyooka sipindipindi hivi na mi nilivyo ukibipu tu nakupigia hapo hapo, siogopi mtu wa aina yoyote, Julai kelele sijui nimekatiwa umeme, maji uwe mkurugenzi wa mji mdogo, halmashauri, miji midogo mradi wa kitaifa sijui nini naomba ujiongeze, vinginevyo ndio kipimo chako kwamba wewe hutoshi,” alisema.

Kamwelwe alisema uzoefu unaonyesha kuwa halmashauri nyingi zimekuwa hazitekelezi bajeti kwa ufanisi katika fedha za program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP).

Alibainisha Halmashauri 128 katika mwaka wa fedha 2016/17 zimetumia chini ya asilimia 50 ya bajeti zao na kati ya hizo Halmashauri 46 zilitumia chini ya asilimia 10 ya bajeti.

Hata hivyo, alisema Halmashauri 56 pekee ndizo zilizotumia bajeti yao kwa zaidi ya asilimia 50.

Kuhusu rushwa, alisema serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kuchukua rushwa au kuwa na viashiria vya kupokea rushwa na kwamba kwasasa Tume ya kuchunguza hali ya miradi ya maji nchini hususan vijijini inaendelea na kazi na inatarajiwa kukamilisha Agosti mwaka huu.

No comments:

Post a Comment