WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii irudi
kwenye maeneo yote yenye migogoro ya mipaka na iungane na Halmashauri za
wilaya ili waweze kutoa majibu kwa wananchi.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana (Alhamisi, Februari 8, 2018) wakati akijibu
swali la mbunge wa Urambo, Bibi Margaret Sitta wakati wa kipindi cha
maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu Bungeni mjini Dodoma.
Bibi
Sitta alitaka kujua Serikali imeweka taratibu na mikakati gani ya
kumaliza migogoro ya mipaka inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya
hifadhi za misitu nchini kwa kuwa wananchi wanahitaji maeneo kwa ajili
ya shughuli za kilimo na mifugo.
Waziri
Mkuu amesema Serikali iliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iweke
vigingi kwenye maeneo yote yanayozunguka hifadhi za misitu ili kuweka
alama zitakazopunguza migogoro ya kuingiliana kati ya wananchi walioko
kwenye vijiji na wahifadhi kwenye maeneo ya hifadhi ya misitu hiyo.
Amesema
maagizo hayo yalitolewa baada ya kugundua kuwa kuna migogoro mingi kati
ya wananchi walioko katika vijiji vya jirani na misitu iliyohifadhiwa
kisheria ambayo ina ramani.
“Lakini
tunatambua kwamba wanapoendelea na zoezi hilo la uwekaji alama, inaweza
kutokea kijiji kikajikuta kipo ndani ya mipaka ya hifadhi na inaweza
kusababisha kutoelewana kati ya wanakijiji na wenye mamlaka ya hifadhi.”
“Tuliwasihi
wanakijiji wakati zoezi hili linaendelea na hata kama kijiji kitajikuta
kimezungukwa na hizo alama, wanakijiji watulie ili kazi ya awali
ikamilike na pale kwenye mgogoro, Serikali itarudi tena kuja kuangalia
mgogoro huo na kufanya tathmini ya kina.”
Amesema
Serikali iliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii inapofanya kazi hiyo
ya kuweka vigingi lazima ishirikishe mamlaka za halmashauri na kijiji
husika na wao washiriki katika zoezi hilo ili kuondoa migogoro isiyokuwa
ya lazima.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali ilishaielekeza Wizara ya
Mifugo na Uvuvi izitumie ranchi za NARCO na kugawa katika vitalu ili
kubaini ukubwa wa eneo iliyonayo ndipo iweze kufanya uamuzi wa kugawa
vitalu hivyo kwa wafugaji.
Ameyasema
hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Nkenge, Balozi Dkt.
Diodorus Kamala aliyetaka kujua taarifa ya kamati iliyoundwa na Serikali
kufuatilia migogoro ya ranchi zilizokuwa chini ya NARCO na wafugaji,
itapelekwa lini bungeni ili iweze kujadiliwa.
Waziri
Mkuu amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliunda tume ya kufuatilia
maeneo yote ya ranchi za Taifa na kuyapima maeneo hayo lakini pia kujua
ni akina nani wanayamiliki maeneo hayo, kubaini kama walipewa kihalali,
na kama ni kweli wanamiliki mifugo yoyote kwenye maeneo tajwa.
Kuhusu
kupelekwa bungeni kwa taarifa ya tume hiyo, Waziri Mkuu amemtaka Waziri
wa Mifugo aikamilishe na kuiwasilisha Bungeni kama taratibu zinavyotaka
ili kuwawezesha wabunge na wananchi wajue dira na mwelekeo wa Serikali
wa namna ya kufuga mifugo hiyo kwa njia ambazo zitawaletea tija lakini
kikubwa zaidi ni kumaliza migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment