Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.
MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imetiliana saini na Kampuni ya Thades ya Ufaransa kuhusu mkataba wa ufungaji wa mitambo ya rada nne za kuongozea ndege ambazo zitawezesha kuongeza mapato ya nchi kwa kuruhusu ndege kubwa zaidi kutua na anga lote la Tanzania litaonekana.
Hivi sasa Tanzania ina rada moja ya kuongozea ndege iliyonunuliwa mwaka 2002 ambayo uwezo wake umepungua kutokana na mabadiliko yanayotokea kwa haraka katika sekta ya usafiri wa anga.
Mradi huo utagharimu Sh bilioni 61.3 utachukua kipindi cha miezi 18 kukamilika, kufungwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere JNIA), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA) na Uwanja wa Ndege Mwanza.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (pichani) alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa utiaji saini huo ambao ulienda sanjali na uzinduzi wa nembo mpya ya TCAA.
Profesa Mbarawa alisema mradi huo, pia utaiwezesha Tanzania kuboresha utoaji wa huduma za kuongoza ndege, kukuza sekta ya usafiri wa anga na hatimaye kuongeza mchango katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Mradi huu ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa na Serikali ya Rais John Magufuli inayodhihirisha nia ya kuimarisha sekta ya usafiri wa anga na kufikia azma ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025,” alieleza Profesa Mbarawa.
Kwa mujibu wake, mchakato huo ulianza muda mrefu, naye aliukuta akaamua kuchukua jukumu hilo kwa uaminifu mkubwa kwani jambo hilo halikuwa rahisi hata kidogo. Alielezea faida ya kuwekwa rada hizo zitawezesha ndege nyingi kupita katika anga la Tanzania kwa kuwa litakuwa ni salama hivyo kuiwezesha serikali kupata mapato, pia katika sekta ya utalii kutakuwa na mapato mengi kwa kuwa ndege kubwa zitaleta watalii nchini.
“Kwenye migodi zinaingia ndege nyingi na kwenye mbuga za wanyama, lakini tumeshindwa kuziona, lakini baada ya kuwekwa rada hizi tutaziona na kuwasiliana na TRA ili kuhakikisha tunapata mapato sahihi,” alisema.
Alisema hivi sasa ndege zinazoruka urefu wa futi 24,500 anga la Tanzania hawazioni, rada za Kenya ndizo zinaziongoza, lakini hizi zikishafungwa hali hiyo itatengemaa. Naye Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alisema mradi huo ni miongoni mwa mipango mikakati iliyopewa kipaumbele cha juu na mamlaka hiyo katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 kwa lengo la kuimarisha uwezo wa Tanzania katika kutoa huduma za kuongoza ndege, kuboresha usalama wa sekta ya usafiri wa anga pamoja na kuongeza mapato yatokanayo na tozo ya huduma za kuongozea ndege.
Alisema ongezeko la ndege zinazotumia anga la Tanzania limesababisha kuwa na mahitaji ya mitambo ya aina hiyo ili kufanikisha taratibu za urukaji ndege kwa kufuata viwango vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
“Kutokana na uwezo wa rada yetu kupungua baadhi ya nchi jirani zilikuwa zimeanza kampeni za kutaka kukasimiwa anga la Tanzania ili kuliongoza, kutokana na kuwa na rada zenye uwezo mkubwa ambazo zilikuwa zinaweza kumulika hata anga la Tanzania,” alisema Johari na kuongeza kuwa jitihada za kuwa na rada mpya za kuongoza ndege zilianza miaka mitatu iliyopita ambapo maombi hayo yalikuwa yakiwasilishwa Serikali Kuu.
No comments:
Post a Comment