Wednesday, September 13, 2017

WALIOMHUSISHA OFISA POLISI NA TUKIO LA LISSU MTEGONI

MSEMAJI WA JESHI HILO, BARNABAS MWAKALUKWA.


JESHI la Polisi linafanya uchunguzi kuwabaini waliohusika kusambaza taarifa zinazodai ofisa wa polisi kuhusishwa katika tukio la kuvamiwa na kujeruhiwa risasi kwa Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, Septemba 7, mwaka huu.

Sambamba na uchunguzi huo, jeshi hilo limewataka wananchi kuacha kutumia mitandao ya kijamii vibaya na badala yake itumike kuelimisha na kuhabarisha jamii juu ya masuala ya maendeeleo.

Msemaji wa Jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam ikiwa siku chache baada ya kutolewa kwa taarifa za ofisa huyo, akidaiwa kuonekana akifanya ukachero Nairobi nchini Kenya, ambako Lissu anapatiwa matibabu.

Mwakalukwa alisema taarifa hizo zilizoenezwa kuanzia juzi ni za uongo na zenye lengo la kumharibia ofisa huyo na jeshi kwa ujumla na kwamba hayuko Nairobi kama ilivyoelezwa.

“Kuhusu safari ya Nairobi, askari huyo alikuwa nchini Kenya kwa mafunzo kuanzia Septemba 4 hadi 8, mwaka huu, aliporejea nchini wakati Lissu alipatwa na mkasa huo Septemba 7 na kufika Septemba 8 alfajiri  mjini Nairobi,” alisema.

“Suala la Lissu liko chini ya uchunguzi ili kuwabaini waliohusika na hatimaye kuwafikisha mahakamani. Ni vyema wananchi na wanasiasa wakaliacha jeshi la polisi lifanye kazi yake bila kuliingilia na kupata ukweli wa jambo hili.”

Aidha, Mwakalukwa aliwatahadharisha wananchi kuwa jeshi hilo kupitia kitengo cha upelelezi wa makosa ya mitandao, linaendelea na uchunguzi wake ili kuwabaini wote waliohusika kusambaza taarifa hizo za uongo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

No comments:

Post a Comment