SPIKA WA BUNGE, JOB NDUGAI.
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amepiga mkwara wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa wanapotaka kupambana naye lazima wajipange na wasimchukulie kirahisi rahisi kwa kuwa hawatammudu.
Ndugai aliyasema hayo bungeni jana baada ya kipindi cha Maswali na Majibu alipokuwa akitoa matangazo mbalimbali kama ilivyo ada.
Alifikia hatua hiyo alipokuwa akijibu shutuma zilizotolewa juzi na Mbunge wa Malindi (CUF), Ali Saleh, kuhusu uamuzi wa Naibu Spika wa kutangaza safu mpya ya viongozi wa CUF wakati kuna uongozi mwingine.
“Mheshimiwa Ali Saleh alisema jana (juzi) hapa ingawa sikuwapo na leo kwenye taarifa ya upinzani amerudia rudia tena kwenye utangulizi maneno yale yale.
Sasa hawa rafiki zangu wanapenda sana kunituhumu, lakini nawaambia kila mtu mumsome vizuri mmwelewe… Am a smart person (niko makini), hivyo mnapokuja kwangu mjipange kidogo msifikiri ufupi huu ni shida,” alisema Ndugai.
Juzi bungeni, Ali Saleh alimhoji Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, kuwa iweje atangaze safu mpya ya uongozi ilhali bado kuna uongozi halali wa chama hicho ndani ya Bunge hilo.
Saleh alisema wabunge wa chama hicho wameshafanya mabadiliko ya uongozi baada ya wabunge wengine kuondolewa bungeni, hivyo kauli ya Naibu Spika kwamba kuna safu nyingine mpya imewashangaza.
“Mheshimiwa Naibu Spika inakuwaje unatangaza kuwa kuna viongozi wapya wakati hakuna sehemu iliyoelezwa kuwa uongozi uliokuwepo umebatilishwa? Sisi tumeshafanya uchaguzi wetu humu na tayari tuna viongozi?“ alihoji Saleh.
Jana, Ndugai alisema kazi yake ni kutangaza na ataendelea kutoa matangazo mbalimbali yanayoletewa na vyama vya siasa kwa kuwa ndiyo kazi yake.
Alisema hahusiki na vikao vya vyama vya siasa, hivyo anapotangaza mabadiliko haoni sababu yoyote ya kubebeshwa lawama na badala yake wajiangalie.
“Mimi leo hii Mbowe akiniletea mabadiliko kuwa amembadili Waziri Kivuli natangaza. Kazi yangu ni kutangaza, maana mnapokaa huko kwenye vikao vyenu mimi si mmoja wa wajumbe. Sasa mnapolalamika kuwa nimefanya maamuzi (uamuzi), maamuzi (uamuzi) yapi au nimeridhia wapi,” alihoji Ndugai.
Juzi, Dk. Tulia aliwatangazia wabunge kuwa Chama cha Wananchi (CUF), kimepata uongozi mpya hali iliyosababisha baadhi ya wabunge kuanza kuhoji uhalali wa uongozi huo mpya.
Kwenye uongozi huo mpya, Mwenyekiti ni Maftah Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini na Katibu wake ni Rukia Kassim Ahmed wakati Mnadhimu atakuwa Maulid Mtulia ambaye ni Mbunge wa (CUF) Kinondoni na Mweka Hazina ni Sonia Magogo.
Dk. Tulia aliwatangazia wabunge kuwa Bunge limepokea barua ya Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Magdalena Sakaya, kuliarifu kuwa wamepata uongozi mpya.
“Waheshimiwa wabunge kwa kawaida bungeni kunakuwa na Kambi Rasmi ya Upinzani lakini vyama navyo huwa vina uongozi wao, hivyo CUF wametuletea safu mpya ya uongozi,” alisema Dk. Tulia.
No comments:
Post a Comment