KUNAFUKUTA! Ndivyo ilivyo, kwani baada ya timu yao kupata sare ya bila kufungana dhidi ya Azam FC wiki iliyopita huku ikiwa na wachezaji kibao wenye kiwango cha juu, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mcameroon Joseph Omog, amepewa mechi tano za kutathimini ajira yake ndani ya klabu hiyo.
Taarifa zilizopatikana jana jijini Dar es Salaam zinaeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo umeonyesha kutoridhishwa na upangaji wa timu unaofanywa na Omog, na kudai ndiyo moja ya sababu ya timu yao kushindwa kupata idadi nzuri ya mabao katika mechi mbalimbali walizocheza kuanzia kipindi cha maandalizi ya msimu huu.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa viongozi wa juu wa timu hiyo, alisema baada ya kufanikiwa kusajili wachezaji wenye uwezo katika idara zote, wanatarajia kuona Simba "haitaabiki" kusaka ushindi na lawama zote wamezihamishia kwa kocha.
Kiongozi huyo alisema mbali na kushindwa kupata mabao mengi, pia kocha huyo analalamikiwa kwa kuchelewa kufanya mabadiliko wakati mechi inaendelea licha ya baadhi ya wachezaji kuonyesha kuwa mechi "imewakataa" na kusababisha mashambulizi kupungua.
"Ni kweli hilo jambo, ameelezwa na amepewa mechi tano na kuanzia ya Mwadui ambayo itachezwa Jumapili, Simba ya sasa haipaswi kushindwa kufunga mabao," alisema kiongozi huyo.
MIKAKATI ILIYOPO
Kocha Msaidizi wa Wekundu hao wa Msimbazi, Jackson Mayanja, aliliambia gazeti hili jana kuwa kikosi chao kinaendelea vizuri na mazoezi, na kwamba wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi mnono katika mechi dhidi ya Mwadui FC itakayopigwa Uwanja wa Uhuru.
"Tunajua huko mbele mambo yanaweza kuwa magumu zaidi na hasa kilichotokea msimu uliopita wote mnajua, tunataka kuona kila mechi tunashinda zaidi ya mabao matatu," alisema Mayanja.
Aliongeza kuwa kila mchezaji ndani ya timu hiyo anafahamu umuhimu wake na wote wamesajiliwa ili kuipa timu matokeo mazuri na hakuna ambaye ni bora kuliko mwenzake.
Baada ya mechi hiyo dhidi ya Mwadui FC, mabingwa hao wa Kombe la FA watasafiri kuelekea Mwanza kuwafuata Mbao FC katika mechi nyingine ya Ligi Kuu Bara itakayofanyika Septemba 21, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba.
No comments:
Post a Comment