Tuesday, September 5, 2017

MGOGORO CUF WAIBUA CHADEMA

Katibu  wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),Wilaya ya Tanga, Jonathan Bahweje, amekerwa na mgogoro kati ya madiwani wa Chama cha Wananchi (CUF) wilayani humo na Mbunge wa Jimbo hilo, Mussa Mbaruk kwa tiketi ya chama hicho, na kutaka umalizwe haraka.

Bahweje alisema mgogoro huo ni hatari kwani usiposhughulikiwa haraka utadhoofisha  mshikamano uliyopo  na maendeleo ya wanajamii wa Tanga kwa ujumla na kukitaka CUF kufanya jitihada za haraka kwa manufaa yake na ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mwishoni mwa wiki, baraza la madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Tanga liliwasimamisha kuhudhuria vikao vinne  na kukatwa posho za vikao  hivyo madiwani wanne wa CUF kwa madai ya kutoka nje wakati mbunge huyo alipopewa nafasi ya kuzungumza.

Madiwani waliyosimamishwa na kata zao kwenye mabano ni Rashid Jumbe (Mwanzange), Khalid Hamza (Duga), Seleman Mbaruk ( Majengo), Mwasabu Ngale (Mabawa) na Abdrahaman Hassan (Msambweni).

Bahweje alisema hali hiyo inatisha na ni mgogoro ambao utatuzi wake unahitaji busara zaidi kutokana na ukweli kuwa wote ni viongozi wenye uwakilishi ndani ya jamii na chama hicho kwa ujumla.

Bahweje aliwataka wanachama wa Chadema Wilaya ya Tanga kujitokeza kwenye chaguzi zinazoendelea ndani ya chama kwa
kugombea nafasi mbalimbali na kupanga safu ya ushindi serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu mwaka 2020.

 Alisema chama hicho kinahitaji wanachama wenye sifa na uwezo kugombea uongozi katika nafasi za ngazi ya msingi na matawi
zinazoendelea ndani ya chama hicho, ili kuunga mkono mipango ya ushindi iliyopo.

No comments:

Post a Comment