Tuesday, September 5, 2017

MO APIGIWA HONI SIMBA


MOHAMMED DEWJI MAARUFU KAMA MO.

WAKATI mfanyabiasha Mohammed Dewji maarufu kama MO, akitajwa kuwa mmoja wa wanachama waliotangaza nia ya kununua asilimia 50 ya hisa za klabu ya Simba, uongozi wa klabu hiyo umeunda kamati ya watu watano (Kamati ya Tenda) kusimamia mchakato mzima wa uuzaji wa hisa hizo.

Kamati hiyo ambayo itakuwa huru katika kufanya kazi zake, itakuwa chini ya Mwenyekiti, Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu, Thomas Mihayo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Dk. Arnold Kashembe, aliwataja wajumbe wengine wa kamati hiyo kuwa ni Wakili Dk. Damas Ndumbaro, Mkurugenzi wa Mikopo ya Elimu ya Juu, Abdulrazaq Badru, Mbunge wa Ilala, Mussa Hassan Zungu pamoja na Mtaalam wa masuala ya Manunuzi , Dk. Yusuph Majjid Nassoro.

Kashembe, alisema kamati hiyo itafanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria zote za manunuzi za nchi na wanategemea itamaliza kazi yake katika kipindi cha siku 45.

“Baada ya kukamilisha mchakato huu wa kutangaza tenda na kupata mnunuzi, kamati hii itawasilisha jina la mshindi ambaye ni lazima awe mwanachama wa Simba, kwa Kamati ya Utendaji ya klabu ambayo wao watafikisha kwa wanachama,” alisema Kashembe.

Alisema mara baada ya kamati hii kutangaza tenda, wanachama wa Simba wenye uwezo watajitokeza kuomba kununua hisa hizo asilimia 50.

Kamati hiyo itakutana kuanzia kesho kujuana na kupanga mipango yao kabla ya kuanza kazi.

Katika mabadiliko yaliyopitishwa kwenye mkutano wa wanachama mwezi uliopita, Simba itauza hisa zake asilimia 50 kwa mwekezaji ambaye ni lazima awe mwanachama wa klabu hiyo, asilimia 10 kati ya 50 zitakazokuwa zimebaki zitagawiwa bure kwa wanachama hai na nyingine 40 zitauzwa kwa wanachama hao.

Aidha, katika hisa hizo asilimia 40 zitakazouzwa kwa wanachama, mwanachama ambaye atakuwa tayari ameshinda tenda ya kununua asilimia 50, hatoruhusiwa yeye wala familia yake kununua hisa hizo.

No comments:

Post a Comment