Tuesday, September 5, 2017

TFF YASIKIA KILIO CHA AZAM


Hatimaye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesikia kilio cha Azam kwa kukubali mechi zake dhidi ya Simba na Yanga kuchezwa usiku kwenye  Uwanja Azam Complex, Chamazi.
Kwa mujibu wa ratiba ya TFF, iliyotolewa leo Jumatatu pamoja na kufanyiwa marekebisho inaonyesha Azam itacheza mechi zake mbili za mzunguko wa kwanza nyumbani dhidi ya Simba na Yanga.

Hii ni mara ya kwanza kwa Azam kuruhusiwa kutumia uwanja wake wa nyumbani inapocheza dhidi ya wapinzani wake hao wa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Azam watakuwa mwenyeji wa Simba kwenye uwanja huo Jumamosi ijayo Septemba 9, kabla ya kuwavaa Yanga hapo Desemba 29 ikiwa ni mechi yake ya mwisho wa mzunguko wa kwanza.

Uwanja wa Azam Complex una vipimo vya mita 110 kwa mita 71 sehemu ya kuchezea, pia una milango mine ya kieletroniki na uwezo wa kuchukua zaidi ya mashabiki 7,000 kwa wakati mmoja.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Januari 31, 2014 lilitoa kibali kwa uwanja wa Azam Complex Chamazi kuchezea mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na CAF na mashindano makubwa ya klabu.

Mbali ya Azam timu nyingine zinazosumbuliwa na tatizo hilo ni Mwadui FC, ambayo wanapocheza na Yanga na Simba hutumia uwanja wa Kambarage badala ya ule wa Uwanja wa Mwadui Complex, wengine ni Mtibwa Sugar wanaotumia uwanja wa Jamhuri badala ya Manungu na Ruvu Shooting inayotumia Uwanja wa Taifa au Uhuru badala ya Mabatini uliopo Mlandizi Pwani.

No comments:

Post a Comment