IBRAHIM AJIBU.
Mshambuliaji mpya aliyesajiliwa na Yanga msimu huu, Ibrahim Ajibu, ameanza kujibu baada ya jana kuwa shujaa kwa kuifungia timu yake bao pekee kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Sabasaba mjini hapa na wageni kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Njombe Mji.
Ajibu alifunga bao hilo katika dakika ya 17 kwa shuti la mpira wa faulo iliyotokana na nyota huyo kuangushwa na umbali wa mita 29 kutoka lango la Njombe Mji.
Bao hilo ni kama lilifunga nyavu za timu zote kwa kuwa pamoja na juhudi ya kila timu kutaka kufunga mabo yalikuwa magumu.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Seleman Kinugani, Yanga walitengeneza nafasi za maana katika kipindi cha kwanza huku wenyeji wakilisakama zaidi lango la Yanga muda mwingi wa kipindi cha pili, lakini uimara wa kipa Youthe Rostand, uliwanyima Njombe Mji nafasi ya kupata bao kutokana na kipa huyo raia wa Ivory Coast kuokoa michomo mingi iliyokuwa ikielekezwa golini kwa Yanga.
Kipindi cha pili Njombe Mji walipata pigo baada ya beki wake, Remy Mbuligwe, kulazimika kukimbizwa hospitali kutokana na kuumia baada ya kugongana na beki wa Yanga, Juma Abdul, kabla ya tukio hilo, Yanga nayo ililazimika kumtoa nje kiungo wake Thaban Kamusoko kufuatia kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Raphael Daudi katika dakika ya 50.
Katika mchezo wa jana, Yanga ilimtumia kwa mara ya kwanza msimu huu mshambuliaji Obbrey Chirwa aliyeingia uwanjani katika dakika ya 56 kuchukua nafasi ya Donald Ngoma.
Baada ya mchezo huo, Kocha wa Yanga, George Lwandamina, alisema wachezaji wake walijituma pamoja na kukumbana na changamoto ya uimara wa Njombe Mji.
"Uwanja pia haukuwa rafiki kwetu, nashukuru tumepata pointi tatu ambalo lilikuwa lengo letu, wapinzani wetu walicheza vizuri hasa kipindi cha pili na kutupa wakati mgumu," alisema Lwandamina.
Kwa ushindi huo, Yanga inayodhaminiwa na Kambuni ya Kubashiri ya SportPesa imefikisha pointi nne baada ya kucheza michezo miwili kutokana na mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dares Salaam, mabingwa hao watetezi kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Lipuli ya Iringa.
Vikosi vilikuwa, Njombe Mji: David Kisu, Agaton Mapunda, Remmy Mbuligwe, Laban Kamboole, Peter Mwangosi, Joshua John, Awadh Salum, Hassan Kapalata/Behewa Sembwana (dk. 80), Notikeli Masasi, Ditrim Nchimbi na David Nakpa/Raphael Siame (dk. 47).
Yanga: Youthe Rostand, Juma Abdul, Gardiel Michael, Andrew Vincent, Kevin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Juma Mahadhi, Thabani Kamusoko/Raphael Daudi (dk. 49), Donald Ngoma/Obrey Chirwa (dk. 56), Ibrahim Ajibu na Emmanuel Martin/Yussuf Mhilu (dk. 70).
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyopigwa jana Uwanja wa Jamhuri Dodoma, Singida United inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri ya SportPesa, iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC.
Mabao ya Singida yalifungwa na Mudathir Yahya dakika ya 26 na Mishel Katsavairo dakika ya 57.
No comments:
Post a Comment