Thursday, August 10, 2017

WANAFUNZI YATIMA WABANWA BODI YA MKOPO



SIKU chache baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kufungua dirisha la mikopo kwa mwaka wa masomo wa 2017/18, sasa imekuja na mbinu mpya za kuwatambua yatima baada ya kutaka kupata uhalali wa vifo vya wazazi wao.

Mkurugenzi  Mtendaji wa Bodi ya Mikopo, Abdulrazaq Badru, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema wanashirikiana na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) kwa ajili ya kuhakiki nyaraka za wanafunzi wanaohitaji mikopo, ambao wazazi wao wamefariki dunia.

“Bodi ya mikopo tumeona ni vizuri kuuarifu umma juu ya suala hili. Lengo ni kuleta ufahamu na kutoa msisitizo kuhusu umuhimu wa kuzingatia hatua hizo,” alisema.

Alisema yatima wanatakiwa kuwasilisha nakala ya cheti au vyeti vya kifo vilivyodhibitishwa na Rita na kwa waliofadhiliwa wanatakiwa kuwasilisha barua kutoka kwa taasisi au mtu aliyemfadhili.

Badru alisema miongozo mingine ni mwanafunzi kuambatanisha fomu ya maombi iliyotiwa saini na kamishna wa viapo, wakili au hakimu na nakala za vyeti vya taaluma zilizogongwa muhuri na kamishna wa viapo na wakili au hakimu.

Alisema mwanafunzi anatakiwa kuwasilisha nakala ya cheti cha kuzaliwa kilichothibitishwa na Rita na nyaraka zingine muhimu zinazohitajika.   

“Hii ni baada ya kufungua dirisha la kuomba mikopo kwa wanafunzi wa mwaka 2017/18 tangu Agosti 6 hadi Septemba 4, mwaka huu.

Na mwongozo umeainisha sifa za msingi za mwombaji ikiwamo lazima awe Mtanzania na awe ameomba kudahiliwa vyuo vikuu vinavyotambuliwa na serikali,” alisema.

Naye Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson, alisema waombaji wote wa mikopo watatakiwa kuhakiki vyeti vya kuzaliwa na vifo katika ofisi za wilaya zilizotoa vyeti hivyo.

“Bodi ya mikopo ni wadau muhimu na tumekuwa tukifanya nao kazi kwa karibu kila mwaka kwa lengo la kuhakiki nyaraka hizo kwa wanafunzi wote,” alisema.

Alisema kwa walio mbali na ofisi zilizotoa vyeti hivyo wanatakiwa kuwasilisha maombi kwa Rita makao makuu kupitia barua pepe uhakiki@rita.go.tz na maombi hayo yaambatanishwe na risiti za malipo ya ada ya uhakiki na nakala ya cheti inayoonyesha vizuri.

Hudson pia alitaja ada ya kufanyia uhakiki huo kuwa ni Sh. 3,000 kwa kila mwanafunzi ambayo inatakiwa kulipwa kupitia benki ya NMB.

No comments:

Post a Comment