ATHUMAN IDDI ‘CHUJI’.
KIUNGO wa zamani wa klabu ya Yanga, Simba na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Athuman Iddi ‘Chuji’ amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia klabu ya Ndanda FC ya mkoani Mtwara.
Awali Chuji ilisemekana anataka kujiunga na Mbeya City, lakini nyota huyo jana alithibitisha kujiunga na Ndanda kwa mkataba huo wa mwaka mmoja.
Akizungumza na Nipashe jana, Chuji alisema jana asubuhi alikuwa akitegemea kuelekea Mtwara kujiunga na timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu.
“Ni kweli, jana nimekutana na viongozi wa timu hiyo wakiwa na makocha na nimesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Ndanda,” alisema Chuji.
Aidha, alisema kwa sasa anajipanga kuhakikisha anaisaidia timu hiyo msimu ujao ili iweze kufanya vizuri.
“Tumepanga kuondoka leo asubuhi hii (jana) kuelekea Mtwara kuungana na wenzangu ambao tayari wapo kwenye maandalizi,” aliongezea kusema Chuji.
Hata hivyo, kusajiliwa kwa nyota huyo kumeleta utata katika kuthibitisha kwani kundi moja lililokuwa limeweka maskani yake Dar es Salaam ndilo lililomsajili kiungo huyo huku lingine ambalo lipo na timu Mtwara likiukana usajili huo.
No comments:
Post a Comment