Thursday, May 18, 2017

SERIKALI YAJA NA MBINU MPYA KUINUSURU IHEFU


Serikali mkoani Mbeya imesema itaanzisha utaratibu mpya wa utoaji adhabu kwa wafugaji wanaoingiza mifugo ndani ya eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha upande wa Ihefu ili kukomesha kabisa tabia hiyo.
Mpango mpya wa utoaji adhabu unaotarajiwa kuanza kutumika na Serikali mkoani hapa ni Kutaifisha mifugo yote itakayokamatwa ikiwa imeingizwa ndani ya Hifadhi na kuuzwa kwa njia ya mnada.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alibainisha hayo alipozungumza na wakazi wa kijiji cha Yala kilichopo katika kata ya Luhanga wilayani Mbarali alipotembelea kijiji hicho kilicho jirani na Hifadhi ambacho miongoni mwa wakazi wake ni wafugaji.
Makalla alisema maamuzi ya kuanzishwa mfumo wa utoaji adhabu kwa wafugaji kupitia kutaifisha Mifugo yamekuja kufuatia mfumo uliokuwa ukitumika awali kuonekana kutotoa funzo kwa baadhi ya wafugaji.
Alisema baadhi ya wafugaji wakorofi ambao kwa adhabu ya kulipa faini kila wanapokamatwa ng’ombe wao hifadhini wamekuwa wakiona haiwaumizi hivyo kulipa na kisha kuingiza tena mifugo yao ndani ya hifadhi.
Aliwataka wakazi wa vijiji jirani na hifadhi kuacha kukaribisha wafugaji wapya wanaoingia kwa kificho wakitokea maeneo mengine na kusababisha mlundikano wa mifugo vijijini kwa kuwa maeneo yaliyopo ya malisho yanatosheleza mifugo iliyokuwepo wakati wa utengaji maeneo kwa ajili ya matumizi ya vijiji husika.

No comments:

Post a Comment