Thursday, July 20, 2017

KAPOMBE OUT MECHI YA STARS VS RWANDAA

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ keshokutwa Jumamosi itapambana na Rwanda katika mchezo wa marudiano wa kufuzu fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) utakaopigwa kwenye Uwanja wa Nyamirambo jijini Kigali bila ya beki wake wa kulia Shomari Kapombe.

Stars iliondoka jana Jumatano jijini Mwanza kuelekea Kigali kupitia Dar es Salaam baada ya kufanya mazoezi kwa siku mbili kwenye Uwanja wa Nyamagana. jijini Mwanza.

Shomari Kapombe aliumia kwenye mchezo wa kwanza na nafasi yake ilichukuliwa na kiraka wa Mbao FC, Boniface Maganga ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuanza kwenye mchezo huo baada ya kufanya vizuri alipoingia kuchukua nafasi yake katika mchezo wa kwanza.

Kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga alisema timu yake imedhamiria kushinda mchezo huo na kufuzu hatua inayofuata.

“Kapombe hatakuwemo, lakini tunaye Maganda (Boniface) na Nyoni (Erasto) pia anaweza kucheza nafasi hiyo hata Kessy pia hali yake inaendelea vizuri. Rwanda ni wazuri na hatukucheza vizuri katikati jambo tulilolifanyia kazi kwa siku mbili,” alisema Mayanga aliyewahi kuifundisha Mtibwa Sugar.

Mshambuliaji wa timu hiyo, Shiza Kichuya alisema wanatakiwa kuwa makini kutumia nafasi watakazopata katika mchezo huo.

“Hii ni mechi ya mtoano na mwalimu amefanya kazi kubwa ya kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza kwenye mechi ya kwanza, muhimu ni kuongeza umakini na kutumia vizuri nafasi tutakazopata. Tuna uwezo wa kuwatoa Rwanda kwao,”alisema Kichuya.

Mshindi wa jumla wa mchezo huo atapambana na mshindi baina ya Sudan Kusini na Uganda ambazo katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Juba zilitoka suluhu.

MCL

No comments:

Post a Comment