Monday, May 22, 2017

WENGER:UTATA KUNIHUSU UMEIGHARIMU ARSENAL NAFASI UEFA

Arsenal watacheza Europa League msimu ujao
Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesema utata kuhusu hatima yake katika klabu hiyo huenda ulichangia kushindwa kwa klabu hiyo kumaliza katika nafsi nne za kwanza katika Ligi Kuu ya England.

Hata hivyo, amesema hakuna anayeweza kutilia shaka kujitolea kwake kufanya kazi yake katka klabu hiyo.

Imekuwa ni mara ya kwanza kwa Arsenal, waliomaliza wa tano, kukosa kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika kipindi cha miaka 20.

Wenger, ambaye mkataba wake unamalizika majira yajayo, hivi majuzi alisema hatima yake itaamuliwa baada ya fainali ya Kombe la FA mnamo 27 Mei.

"Nimekataa klabu zote zilizonitafuta kutoka pande mbalimbali duniani," Mfaransa huyo wa miaka 67 alisema.

Wenger amekuwa kwenye usukani Gunners tangu 1996 ambapo ameshinda mataji matatu ya Ligi ya Premia na Vikombe sita vya FA, lakini mashabiki wa Arsenal msimu huu wamekuwa wakimtaka ajiuzulu.

"Ninamini tangu Januari tumecheza katika mazingira magumu sana kwa sababu mbalimbali," aliongeza.

"Baadhi yenu mnajua hilo na hilo ni jambo ngumu sana kwa wachezaji - na kuna baadhi ya sababu ambazo tutazizungumzia siku nyingine.

"Kiakili, hali ilikuwa ngumu sana. Mambo yamekuwa magumu, ndio, na bila shaka hali yangu imechangia hilo lakini huwezi kutilia shaka utaalamu wangu au kujitolea kwangu."

Mabango yenye ujumbe wa kumtaka Wenger ajiuzulu

Arsenal walilaza Everton 3-1 Jumapili lakini kwa sababu Liverpool walilaza Middlesbrough, Gunners walimaliza alama moja nyuma ya klabu hiyo ya Jurgen Klopp iliyomaliza nafasi ya tano.

Wenger, ambaye klabu yake itakutana na mabingwa wa Ligi ya Premia Chelsea katika fainali ya Kombe la FA alisema inasikitisha sana kwamba Arsenal haitakwua ikicheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.

Aliongeza: "Tulifanya kazi yetu kwani wewe ni mtaalamu na sehemu ya kazi yako kama mtaalamu ni kuendelea kufanya kazi kama mtaalamu hata mazingira yanapokuwa magumu."

Meneja wa zamani wa Manchester United Sir Alex Ferguson ambaye mara kwa mara walikuwa na uhasama na Wenger alipokuwa Old Trafford, ambapo alishinda mataji 13 ya Ligi amemtetea Wenger.
Ferguson alikuwa mkufunzi Man Utd kwa miaka 26 naye Wenger sasa yupo Arsenal kwa mwaka wake wa 21.

"Kwa sasa, bila shaka, ukizingatia presha ya kushangaza ambayo Arsene anakabiliwa nayo, nashangaa iwapo huwa wanatambua kazi nzuri ambayo amewatendea," Ferguson aliambia Sky Sports.

"Jambo zuri zaidi kumhusu ni kwamba; amefanikiwa kujitoa kwenye kichaka hicho cha lawama kwa miezi kadha sasa, na hajawahi kusalimu amri. Amepitia mengi, ameonesha kujitolea kwake, na ukakamavu fulani. Nafikiri ukiangalia hilo, ustadi na kiwango chake, sina uhakika kwamba watawahi kumpata meneja mwingine kama yeye.

No comments:

Post a Comment