Serikali
imeahidi kuendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wazalendo katika
utekelezaji wa miradi mikubwa lakini imewaonya wale ambao wamekuwa
wakitekeleza miradi chini ya viwango vilivyowekwa kwenye mikataba.
Hayo yalisemwa jana mjini Dodoma na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa makandarasi ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB).
Samia
aliagiza kuwa miradi yote ya thamani isiyozidi Sh bilioni 10 wapewe
wakandarasi wa ndani hasa kwa miradi inayotekelezwa kwa fedha za ndani
kwani wakandarasi hao watasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania
na kuongeza uwekezaji ndani ya nchi.
Alisema
kuwapa miradi mikubwa wakandarasi wazalendo kuna faida kubwa kwani
kutasaidia kuwajengea uwezo hivyo kuweza kushindana na wakandarasi wa
nje hivyo fedha nyingi za serikali kubaki ndani.
“Tanzania
bora na yenye viwanda itatokana na wakandarasi bora na wenye uzalendo,
hatuwezi kufikia huko tunakotaka kwenda wakati miradi mikubwa ya ujenzi
inafanywa na wakandarasi wanje…. miradi ni yetu na fedha ni zetu hivyo
lazima tuwape nyinyi,” alisema.
Aidha,
aliwataka wakandarasi wazalendo wakamilishe kazi kwa wakati na kwa
ubora unaotakiwa pale wanapopewa miradi ili wajenge uaminifu kwa
serikali kuendelea kuwaamini na kuwapa miradi mikubwa.
Makamu
wa Rais aliwaonya baadhi ya wakandarasi wanaoshirikiana na maofisa wa
serikali kuongeza gharama kubwa za ujenzi wa miradi kwa misingi ya
rushwa hali ambayo imekuwa ikifuja fedha za serikali.
“Jamani
kwenye mkutano huu tujitathimini na tuanze upya maana kuna wenzetu
ambao hawana maadili na wanaendekeza rushwa, serikali ikitumia taasisi
zake inatekeleza miradi mikubwa kwa gharama ndogo lakini nyinyi wengine
mnaweka gharama kubwa ambazo si halisi,” alisisitiza.
Aliipongeza
CRB kwa namna inavyoendelea kuratibu kazi za wakandarasi wazawa huku
akiitaka kuendelea kuwajengea uwezo ili watekeleze miradi mikubwa kama
kampuni ya nje.
“CRB
mmefanyakazi kubwa sana kuandaa mkutano huu na kwa kuwa mmekutana hapa
naomba mjadiliane kwa uwazi na muelezane ukweli kuhusu changamoto
mlizonazo na namna mtakavyozitatua na sisi serikali mkituletea maazimio
yetu sisi tunaahidi kuyafanyia kazi,” alisema.
Waziri
wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Makame Mbarawa, yeye alisema
asilimia 75 ya madeni ya wakandarasi yameshalipwa na yaliyobaki
yatalipwa wakati ukifika na aliwaomba wawe wavumilivu wakati huu.
“Msidhani
serikali imewasahau, tunafanya kazi kwa bidii kuhakikisha wote mnalipwa
kwa sababu sisi tunaamini na tunafahamu kwamba ili makampuni yenu
yaendelee lazima mlipwe hela zenu hivyo endeleeni kuchapa kazi hela
zilizobaki zinakuja,” aliahidi Profesa Mbarawa.
Mwenyekiti
wa CRB, Consolata Ngimbwa, aliomba serikali iharakishe malipo ya
wakandarasi kwani wengi wao wako kwenye hali mbaya kifedha. Alisema
baadhi ya wakandarasi walifariki dunia kutokana kabla hatajalipwa
malimbikizo ya madeni wanayoidai serikali baada ya kukamilisha miradi
mbalimbali ya ujenzi.
Alisema
wakandarasi wengi wazalendo wana uwezo mkubwa wa kutekeleza miradi
mikubwa ya ujenzi hivyo aliiomba serikali iweke kipaumbele kwa kuwapa
miradi hiyo.
Vile
vile, aliwageukia wakandarasi ambao wamekuwa na kawaida ya kutekeleza
miradi chini ya kiwango na wengine kutokomea mara baada ya kulipwa fedha
za awali za ujenzi.
Msajili
wa CRB, Rhoben Nkori aliwataka wakandarasi kutekeleza miradi wanayopewa
na kuahidi kuwa bodi yake itaendelea kuhakikisha mkandarasi asiye na
viwango anafutiwa usajili.
No comments:
Post a Comment