Thursday, May 4, 2017

WAZIRI MKUU:MAJIJI YOTE KUJENGWA BARABARA ZA KISASA

Waziri mku Kassim Majaliwa amesema Serikali ina mkakati wa kufanya Majiji yote nchini yawe na barabara za viwango vya kimataifa na zinazopitika kwa urahisi.

“Tumeanza kujenga barabara za kisasa katika jiji la Arusha ambalo ni jiji la utalii, tutakwenda Mwanza na Dar es Salaam kwa kujenga barabara zenye njia za juu (flyovers) zikiwemo za magari na za waenda kwa miguu,” amesema.

Ametoa kauli hiyo Alhamisi, Mei 4, 2017 wakati akizumngumza na wananchi wa Tengeru, wilayani Arumeru, mkoani Arusha mara baada ya kukagua barabara ya Sakina- Tengeru yenye urefu wa km. 14.1 ambayo itakuwa na njia nne za magari.

“Nimekuja kukagua ujenzi wa barabara hii ya Sakina hadi Tengeru lakini mkandarasi akimaliza anajenga barabara nyingine ya kilometa 42.1 na hivyo hapa Arusha tutakuwa na kilometa 56.5 za awamu ya kwanza,” alisema.

Alisema maboresho ya barabara za Jiji la Arusha yanafanyika ili kuwezesha wafanyabiashara kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi na viwanda vitakapoanza kujengwa, itakuwa hawana shida ya mawasiliano.

Akizungumzia tatizo la uhaba wa ardhi aambalo lililibuliwa na mbunge wa Arumeru Mashariki, Bw. Joshua Nassari, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw, Mrisho Gambo aendelee na zoezi la kuuzungukia mkoa wake ili kubaini maeneo yenye matatizo sugu.

Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo kwa Waziri Mkuu, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Eng. Mgeni Mwanga alisema ujenzi wa barabara hiyo ambao ulianza Juni 2015, unatarajia kukamilika Juni 2018.

“Ujenzi wa barara ya Sakina –Tengeru ni wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa km. 230 ya kutoka Arusha –Holili- Taveta –Voi ambayo ujenzi wake unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 139.34. Ujenzi huo unagharimiwa na Serikali ya Tanzania pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Sambamba na barabara hiyo, Eng. Mwanga alisema mkandarasi wa barabara hiyo ataanza kujenga barabara nyingine ya km. 42.1 inayoanzaia Usa River hadi Kisongo kwa kiwango cha lami ambayo itakuwa na madaraja saba wakati ile ya Sakina hadi Tengeru ina madaraja makubwa mawili.

Naye mbunge wa Arumeru Mashariki, Bw. Joshua Nassari alisems uhaba wa ardhi bado ni tatizo kubwa kwenye wilaya hiyo kiasi kwamba hawana hata eneo la kujenga shule au zahanati.

“Maeneo yote yameuzwa na wenyeviti wa vijiji na madiwani, hivi sasa ukitaka kujenga shule au zahanati hakuna eneo hata moja. Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba utusaidie kufuatilia suala hilo licha ya kuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi alishakuja na kuelezwa hali halisi ilivyo,” alisema.

No comments:

Post a Comment