SERIKALI imewataka wakandarasi nchini kuwafichua maofisa wa serikali ambao wamekuwa wakiwaomba rushwa ili wawapatie zabuni za ujenzi wa miradi. Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Joseph Nyamhanga, wakati akifunga Mkutano wa Mwaka wa Mashauriano kwa Wakandarasi mjini Dodoma.Mkutano huo uliofunguliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, uliandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), na ni wa kila mwaka ambapo wakandarasi hukutana na kuzungumzia changamoto zinazowahusu na kuziwasilisha serikalini. Nyamhanga alisema kuna umuhimu mkubwa wa kushirikiana kupambana na rushwa kwenye utoaji wa zabuni kwani imekuwa ikisababisha miradi kuchelewa ama kutekelezwa kwa kiwango cha chini.“Kwenye hili naomba muipe ushirikiano mkubwa CRB na serikali tuwabaini hawa watu maana wanakwamisha ustawi wa miundombinu yetu, watajeni hawa watu ili twende mbele kwa kasi,” alisisitiza Nyamhanga. Kuhusu madeni ya wakandarasi, Nyamhanga aliwathibitishia wakandarasi kuwa serikali ina nia njema ya kulipa madeni yote ya wakandarasi na kwa wakati. Alisema kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 serikali ilitenga Sh trilioni 1.006 kwa ajili ya kuwalipa wakandarasi wa ndani na kwamba miongoni mwa fedha hizo Sh bilioni 406 ni fedha zilizotoka kwenye mfuko wa barabara.“Serikali ina dhamira ya dhati kabisa kuwapa wakandarasi wa ndani miradi inayotekelezwa kwa fedha za ndani tumeshaanza na tunaendelea ila mkipewa kazi timizeni mikataba na mzingatie uadilifu kama mlivyofundishwa kwenye mkutano huu,” alisema. “Nawapongeza sana CRB kwa kuandaa mkutano huu ambao kwa kweli umefana sana, mnafanya kazi nzuri na endeleeni kuwasimamia hawa wakandarasi ili kuhakikisha kazi zinakuwa za viwango,” alisema Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), Consolata Ngimbwa, alisema kutozingatiwa kwa Sheria ya Manunuzi ya Umma imekuwa kikwazo kwa wakandarasi wengi kupata zabuni za ujenzi hivyo waliazimia kuwa sheria hiyo ifuatwe.Alisema pia wameazimia kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iendelee kutoa elimu ya kodi ya zuio (withholding tax) kwa wakandarasi, kwani wengi wao bado hawajaielewa vizuri. Alisema CRB itaendelea kuratibu mafunzo ya wakandarasi kwa kanda na wameazimia, kuwa wakandarasi wanapaswa kuzingatia maadili kazini na watekeleze miradi kwa ubora unaotakiwa kwenye mikataba yao.Alisema wameazimia kuwa mamlaka zinazotoa zabuni zisitangaze zabuni kabla ya kupata fedha kwani ucheleweshaji wa malipo kimekuwa kikwazo kikubwa kwa ustawi wa wakandarasi nchini. Alisema mapendekezo hayo yatawasilishwa serikalini siku chache zijazo na kwamba wakandarasi wanaamini kuwa serikali sikivu ya awamu ya tano itafanyia kazi mapema ili kustawisha shughuli za wakandarasi nchini.
No comments:
Post a Comment