Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameitumia salamu za rambirambi familia ya mmoja wa Waasisi wa Taifa la Tanzania Ndg. Paul Sozigwa aliyefariki dunia jana tarehe 12 Mei, 2017 Jijini Dar es Salaam.
Katika Salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amesema Marehemu Paul Sozigwa atakumbukwa kwa utumishi wake uliotukuka kwa Taifa, uchapakazi na uadilifu.
“Natambua kuwa Marehemu Paul Sozigwa ni miongoni mwa Waasisi wa Taifa letu ambao walijitoa kwa dhati kuipigania nchi yetu kabla na baada ya uhuru, alishirikiana na Waasisi wengine wa Taifa letu akiwemo Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizolikabili Taifa letu baada ya uhuru zikiwemo kupiga vita umasikini, ujinga na maradhi ndani ya Chama na Serikali, hakika tutazienzi juhudi zake”amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameitumia salamu za rambirambi familia ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ndg. Said Mwambungu aliyefariki dunia jana tarehe 12 Mei, 2017 katika hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amesema Marehemu Saidi Mwambungu atakumbukwa kwa uchapakazi wake, busara, uongozi mahiri, na uzalendo wake kwa Taifa alipokuwa kiongozi ndani ya Serikali na katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Ndg. Said Mwambungu alikuwa ni kiongozi wa aina yake, moyo wake wa upendo ulimwezesha kufanikiwa katika kazi zake nyingi, siku zote alipigania maendeleo ya wananchi na hakushindwa kutatua jambo kwa njia ya mazungumzo, hakika tutaukumbuka na kuuenzi mchango wake” amefafanua Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewapa pole nyingi wanafamilia, wanachama wa CCM, na wananchi wote walioguswa na vifo hivyo na amewaombea wapumzike mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment