Wednesday, March 22, 2017

VIGOGO MSD WARUKA MAELEZO


VIGOGO wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), akiwamo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Cosmas Mwaifwani na Kaimu Meneja Manunuzi, Frederick Rubanga jana walikana maelezo ya awali dhidi ya shtaka la matumizi mabaya ya madaraka na kusababisha Kampuni ya H.H Hillal Ltd kupata faida ya Sh. milioni 482.2.


Kesi hiyo ilisikilizwa maelezo ya awali jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, iliyokuwa imeketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.



Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Aneth Mavika alidai kuwa kati ya Machi Mosi na 19, 2013 washtakiwa wakiwa Makao Makuu ya MSD yaliyopo Temeke, kwa nafasi zao walitumia madaraka yao vibaya kwa kuandaa na kusaini mkataba namba moja wenye kumbukumbu MSD/003/Q/G/2010/1011/60 wa Machi mosi, 2013.



Pia alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji na wa pili ni, Kaimu Meneja Manunuzi wa MSD.
Washtakiwa walikiri anuani na nyadhifa zao, lakini walikana tuhuma zote zinazowakabili.



Kesi hiyo namba 102 ya 2017 itaanza kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa Jamhuri Aprili 18.



Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya Machi mosi na 19, 2013 katika ofisi za MSD zilizopo Temeke, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walitumia madaraka yao vibaya kwa kufanya mabadiliko ya mkataba na kusababisha Kampuni ya H.H Hillal Ltd, kujipatia faida ya Sh. 482,266,000.


Washtakiwa waliposomewa mashtaka yao walikana na wako nje kwa dhamana.

No comments:

Post a Comment