Wanasheria
wawili wa jijini Dar es Salaam, Tundu Lissu na Lawrence Masha wamesema
wataiomba mahakama kuwajumuisha kama wadaiwa katika kesi za kupinga
uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) walizodai
zimefunguliwa jijini Dar es Salaam na Dodoma.
Lissu,
ambaye ni mbunge wa Iramba na mwanasheria wa Chadema, na Masha
(mwanachama wa Chadema na waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani) wamedai
kuwa kesi hizo mbili zimefunguliwa Mahakama Kuu na Godfrey Wasonga mjini
Dodoma na Onesmo Mpinzile jijini Dar es Salaam, wakitaka uchaguzi huo
uzuiliwe.
Mawakili hao wamewahi kupambana katika kesi mbili tofauti zilizohusu vyama vya CCM na Chadema.
Wasonga
aliwahi kupambana na Lissu katika kesi iliyofunguliwa na wanachama
wawili wa CCM mjini Dodoma waliopinga ushindi wa mbunge huyo wa Singida
Mashariki katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, wakati Mpinzile alipambana na
mwanasheria huyo wa Chadema aliyekuwa akimtetea mbunge wa Kilombero,
Peter Lijualikali ambaye amehukumiwa miezi sita jela.
Hata hivyo, Wasonga alisema jana kuwa hajafungua kesi ila anakusudia kufanya hivyo.
Hatua
ya Lissu, ambaye ni mwanasheria mkuu wa Chadema, kuchukua fomu ya
kuwania urais wa TLS akisema imechagizwa na kauli ya Rais John Magufuli
dhidi ya mawakili, ilibadili upepo wa uchaguzi huo na kumlazimu Waziri
wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe kuuzungumzia akisema Serikali
haitavumilia kuona chama hicho kinajiingiza katika siasa.
TLS
imekuwa ikafanya uchaguzi kila mwaka, lakini umekuwa hauna harakati
kubwa kama ulivyo wa mwaka huu. Tayari TLS imepitisha wagombea urais,
wakiwamo Lissu na Masha.
Mbali
na kuwa mawakili, Masha na Lissu, ambao wote wanawania urais, ni
wanachama wa Chadema, jambo linaloonekana kuchochea mjadala wa siasa
kuingia katika chama hicho.
Lakini,
mgombea mwingine, Godwin Mussa Mwapongo, pia ni kada wa CCM aliyechukua
fomu za kuwania kupitishwa na chama hicho kugombea urais mwaka 2015
ingawa hakufanikiwa. Mgombea mwingine ni Victoria Mandari.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Lissu alisema wamepata wasiwasi kuwa huenda
kukawa na njama za washtakiwa katika kesi hiyo, ambao ni TLS na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kutojitetea vya kutosha na hivyo kukubali
mashtaka ili uchaguzi huo uzuiwe.
Alisema
ili hali hiyo isijitokeze, wataiomba masjala ya Mahakama Kuu iliyopo
Dar es Salaam, iwaunganishe katika kesi hizo kama wadaiwa.
“Uchaguzi
ukizuiwa, maslahi yetu sisi tunaogombea yatakuwa yamevurugwa
kwelikweli. Kwa sababu hiyo na kwa mujibu wa taratibu zinazoruhusiwa
kisheria, sisi ambao tunagombea na wapigakura wanaotaka, tutapeleka
maombi haraka ili tuunganishwe kwenye kesi zile kama wadaiwa,” alisema Lissu.
“Tutanunua
ile kesi, kusije kukawa na njama za uongozi wa sasa wa TLS kuendelea
kuongoza baada ya muda wao wa kikatiba kuisha na kusije kukawa na njama
ya kuzuia uchaguzi na wale ambao wanataka kuvuruga TLS wakafanikiwa.”
Lissu
alisema lengo jingine ni kutaka masuala ya uchaguzi huo yasije
yakaamuliwa nyuma ya migongo yao au juu ya vichwa vyao na hivyo wanataka
kupata fursa kamili ya kuiambia mahakama kwanini maombi hayo ya kuzuia
uchaguzi hayana msingi wowote.
Aliongeza
kuwa mawakili hao walioamua kuweka mapingamizi ni wanachama wa TLS na
walikuwa na nafasi ya kuweka mapingamizi baada ya kamati ya uteuzi
kutangaza majina ya wagombea.
“Kulikuwa
na kipindi cha karibu wiki mbili cha kuweka mapingamizi dhidi ya
wagombea walioteuliwa, fursa hiyo mwisho wake ilikuwa Machi 15 mwaka
huu, lakini hakuna hata mmoja wao aliyeweka mapingamizi hayo. Itabidi
tuwahoji,” alisema.
Kwa
upande wake, Masha alisema hakuna mtu hata mmoja kati ya wagombea wote
wa urais aliyeamua kuingia na kugombea kwa sababu za kisiasa.
Masha
alisema licha ya kuwa hana nafasi ya uongozi Chadema, ni mwanachama
aliyekuwa wa kwanza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya urais kabla Lissu
hajachukua fomu hiyo.
Alisema kama kungekuwa na mbinu za kisiasa, yeye na Lissu wasingechukua fomu ya kuwania nafasi moja.
“Lissu
alikuja kuchukua fomu baada ya muda wa kushiriki katika uchukuaji wa
fomu kuongezwa, kama tungekuwa na njama ya kisiasa isingekuwa rahisi kwa
Lissu na mimi wote kuchukua fomu kugombea nafasi moja,” alisema waziri huyo wa mambo ya ndani wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Masha alisema chama hicho kinaongozwa kwa mujibu wa sheria na kwamba hakina uhusiano wowote katika masuala ya kisiasa.
Kuhusu
matukio yaliyojitokeza Lissu alisema anashangaa kuona Serikali
inaingilia suala la uchaguzi wa TLS, akisema hii ni mara ya kwanza tangu
kuundwa kwake, zaidi ya miaka 60 iliyopita.
“Ni
mara ya kwanza kwa Serikali kuingia moja kwa moja katika suala la nani
anapaswa kuwa kiongozi wa chama hiki. Hii haijawahi kutokea tangu TLS
ilipoanzishwa 1954,” alisema.
Alisema
chama hicho kinaongozwa kwa mujibu wa sheria na kwamba kuwa wanachama
au viongozi wa vyama vya siasa, hakuna maana yoyote ile TLS.
“Linapokuja
suala la uchaguzi wa TLS nafasi zangu zote nilizonazo hazina maana.
Kitu pekee chenye maana ni je wewe ni wakili mwenye sifa zote
zinazotakiwa ili kuweza kugombea nafasi unayotaka kugombea katika chama
cha mawakili,” alisema Lissu.
“Nadhani
Dk Mwakyembe anayafahamu haya, kama atakuwa hayafahamu ni bahati mbaya
sana. Wapiga kura ndio waamuzi wa mwisho kwenye uchaguzi huu. Hatutaki
baraka za yeyote.”
No comments:
Post a Comment