Wednesday, March 22, 2017

JOTO LA UCHAGUZI LAANZA KUMLAINISHA KENYATTA

RAIS UHURU KENYATTA.

Tarehe 8 Agosti mwaka huu Wakenya watatumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wapya akiwamo rais. Wanasiasa, Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo (IEBC) na wananchi wanaendelea kujiandaa kwa ajili hiyo.

Kadri siku zinavyozidi kusonga joto la uchaguzi huo linazidi kupanda, na hivi sasa wanasiasa wameanza kujisogeza sogeza karibu na wananchi kwa kutoa maneno matamu.

Rais Uhuru Kenyatta aliyeingia kwa mara ya kwanza Ikulu mwaka 2012 ameanza kuwapa Wakenya maneno matamu ya kuwalainisha ili mwezi Agosti wampe muhula wa pili ambao ni wa mwisho kwake.

Mzozo wa madaktari ulioanza mwezi Desemba mwaka jana unaonekana kuanza kumpa kiwewe Kenyatta kwa kuamini kuwa athari zilizotokana na mgomo huo zinaweza kumwangukia yeye kwenye uchaguzi huo.

Ingawa mwenyewe amekaririwa mara kadhaa huko nyuma kwamba hababaishwi na mgomo huo, lakini kadri siku za uchaguzi zinavyokaribia, Kenyatta amekuwa akitoa maneno matamu matamu kwa Wakenya.

Moja ya kauli zinazoashiria kuwa Rais Kenyatta ameanza kuonja joto la Uchaguzi Mkuu wa Agosti ni ile aliyoitoa wiki iliyopita ya kutaka kupunguzwa mishahara ya wabunge na maafisa wakuu akisema suala hilo limechangia kuzuka kwa migomo ya wafanyakazi.

Rais Kenyatta aliyasema hayo alipohutubia kwenye kikao cha pamoja cha Bunge la Taifa na Baraza la Senate katika hotuba yake ya mwisho ya kipindi chake cha kwanza uongozini na kuongeza kuwa viwango vya juu vya mishahara ya wabunge vimesababisha migomo ya wafanyakazi wa sekta nyingine kutaka nyongeza za mishahara.

Hotuba ya Kenyetta ilisheheni majibu ya maswali yanayoulizwa na upinzani kila uchao kuanzia ufisadi, ufujaji wa fedha za umma, kuzorota kwa huduma za afya, elimu na usalama.

Kwenye mkutano huo, Uhuru alijivunia kupungua kwa visa vya mashambulizi ya magaidi nchini, kuongezwa kwa idadi ya maafisa wa usalama na ukuaji wa uchumi ambao amesema umekuwa juu ya kiwango cha makadirio ya taasisi za kimataifa cha asilimia tatu kwa mwaka.

Rais Uhuru alitaja mmoja baada ya mwingine miradi ambayo serikali yake imetimiza katika kipindi cha miaka minne uongozini.

Lakini pamoja na yote kauli iliyoibua hisia ni ile ya kutaka mishahara ya wabunge na maafisa wakuu wa serikali ipunguzwa.
Mishahara ya vigogo ipunguzwe

Kauli ambayo ilitafsiriwa kama janja yake ya kampeni, Uhuru alisema viwango vya juu vya mishahara ya wabunbe vimewafanya wafanyakazi katika sekta nyingine kupigania nyongeza za mishahara.

Huku zikiwa zimesalia siku 145 Uchaguzi Mkuu kufanyika Rais Uhuru Kenyatta amechukua fursa ya hotuba hiyo kujipigia upatu ili aweze kuchaguliwa tena kwa kipindi cha pili.

Kinyume na hotuba ya mwaka uliopita, hotua ya mwaka huu haikukatizwa na wabunge wa upinzani kama walivyokuwa wameapa kufanya ikiwa Rais hangeomba msamaha wananchi kwa matamshi yake ya matusi katika siku za hivi karibuni.

Rais Kenyatta amesema kwamba serikali yake imejitolea kuhakikisha uchaguzi wa huru na haki na kuiomba Idara ya Mahakama kutotatiza matayarisho ya uchaguzi ujao.

Tayari kesi kadhaa ziko mahakamani kupinga utaratibu wa tume ya uchaguzi nchini tume ya huru ya uchaguzi nchini humo IEBC.

Rais Uhuru Kenyatta amekumbana na upinzani mkali katika kipindi chake cha kwanza kinachomalizika mwezi wa nane mwaka huu akilaumiwa kwa kukithiri kwa ufisadi, kuzorota kwa usalama na kupanda kwa gharama ya maisha.

Baada ya kulihutubia taifa kiongozi huyo alifungua rasmi jengo la Baraza la Senate na kusema ufunguzi wa ukumbi wa Senete ni ishara ya kuimarika kwa mamlaka ya ugatuzi.

Raila Odinga atamshinda Kenyatta?

Raila Odinga ndiye amekuwa akionekana tishio kwa Uhuru Kenyata na vyama tawala kwenye chaguzi mbalimbali ingawa bado hajawahi kufanikiwa kupenya na kuingia Ikulu.

No comments:

Post a Comment