Tuesday, February 28, 2017

MTOTO AFUNGUKA MAZITO JINSI BABA YAKE ALIVYOUA MKE,NA YEYE MWENYEWE KUJIUA

Dar es Salaam. Hassan Mohammed, ambaye baba yake Mohammed Mohammed (46) aliua mkewe Sophia (36) na yeye kujiua, amesimulia jinsi baba yake alivyokuwa akimweleza matatizo yake na alivyotekeleza mauaji hayo.

Mohammed alifanya tukio hilo Alhamisi wiki iliyopita na kuacha ujumbe wa kutaka kifo chake na mkewe kisihusishwe na mtu yeyote, kwani huo ni uamuzi aliokuwa ameufanya muda mrefu.

Katika tukio hilo, Mohammed aliacha ujumbe wenye jumla ya kurasa 80 uliokuwa umebeba sababu za kifo chake na zilitolewa katika nakala sita ambazo zilielekezwa kwa majirani, mama mkwe, mjomba wake, polisi na mwanaye wa kiume anayeishi Masasi.

Marehemu hao walizikwa jana Boko jijini Dar es Salaam. Mtoto wake wa kwanza Hassan (25) akizungumzia mauaji hayo alisema mara nyingi baba yake alikuwa akimwambia kuna mwanaume alikuwa akihisi ana uhusiano na mke wake, lakini kila alipomuuliza mkewe alikuwa akimkatalia na kusema siyo kweli.

Alisema Jumatano mchana wiki iliyopita Mohammed alirudi nyumbani bila taarifa na kumkuta Sophia akiwa amekaa na huyo mwanaume ndani kwake.

“Alipowaona alijaribu kumuhoji maswali ili aweze kujua ukweli juu ya suala hilo, lakini mwanaume yule aliamua kuondoka bila kuongea chochote na kadri alivyozidi kuuliza hakupewa jibu la aina yoyote zaidi ya kuambiwa kuwa ni kaka yake.”

Alisema hakuchoka kwani siku yenyewe ya tukio (Alhamisi) saa mbili usiku aliporudi nyumbani na wakiwa tayari wameshakula chakula cha jioni, alijaribu tena kumuuliza juu ya yule mwanaume ndipo alipoanza kufokewa na mkewe pasipo kupata jibu linaloeleweka.

Hassan alisema baba yake alipatwa na hasira na kumpiga mwanamke huyo huku mlango wake akiwa ameufunga na kufungulia sauti kubwa ya redio ili majirani wasisikie. “Baada ya tukio marehemu Mohammed alitoka kwenda kwa shemeji yake mama Haji majira ya saa nne usiku na kumgongea lakini alipochelewa kufungua alisukuma mlango kwa nguvu na kuingia na alionekana kuwa mtu mwenye hofu na kukosa cha kuongea. “Baada ya muda kidogo aliwaambia kuna wageni na angetaka waje walale kwake (Mama Haji) kwa sababu nyumbani kwake hakuna nafasi ya kuwaweka.”

Alisema Mama Haji alikubali na ilimlazimu kukaa nje akisubiri wageni mpaka saa sita usiku na asimuone yeye wala wageni alioambiwa watakuja, ndipo aliposikia kuwa shemeji yake kajinyonga siku iliyofuata asubuhi.

Hassan alisema saa nne usiku siku ya Alhamisi alipigiwa simu na shangazi yake akiambiwa kuwa baba yake amemuua mwanamke anayeishi naye na tayari yeye mwenyewe anasubiria kufa kwani ameshakunywa chupa alizokuwa amesaga, sumu ya panya huku akimwambia anaona vyote vinamchelewesha kufa hivyo anaenda kujinyonga.

“Shangazi alijaribu kumsihi asijiue lakini alimwambia hayuko tayari kuendelea kuishi kwani yaliyompata ni mengi zaidi na alimuomba sehemu atakayozikwa mke wake na yeye azikwe hapo,” alisema Hassan.

Alisema baba yake alimwambia shangazi yake kuwa wadogo zake wote anawaacha juu yangu niwaangalie niwatunze na kuwasomesha.

Alisema baba yake amewahi kuoa wanawake wawili kwa ndoa ambao alizaa nao watoto wanne, wa kike wawili na wa kiume wawili pia amewahi kuzaa na wanawake wawili nje ya ndoa ambaye mmoja ana mtoto wa kiume pekee, huku mwingine akiwa na watoto wawili na kufanya jumla ya watoto kuwa saba.

Alisema katika maisha yake alikuwa rafiki wa karibu sana na marehemu baba yake kiasi cha kuwa anamuomba ushauri kwa baadhi ya mambo yanayotokea ndani ya familia na yeye amekuwa akimshauri na kumsihi kila mara juu ya maamuzi aliyokuwa anataka kuyachukua huku akimshauri ni bora ampe talaka mwanamke huyo ili aweze kuishi kwa amani.

“Mara nyingi baba alikuwa anakataa kutoa talaka kwa kile anachodai kuwa amechoka kuoa kila mara na hataki kumuacha na kuanza kutafuta mke mwingine wa uzeeni,” alisema Hassan.

No comments:

Post a Comment