Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 16 Machi, 2017 ametembelea eneo la ujenzi wa Ikulu Chamwino
Mkoani Dodoma na kuwahakikishia wananchi kuwaatahamia Dodoma hivi
karibuni kama alivyoahidi.
Mhe.
Rais Magufuli ambaye ameongozana na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa
Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenister Joakim Mhagama na Katibu Mkuu
Kiongozi Balozi John Kijazi amesema pamoja na majengo ya Ikulu Serikali
itajenga miundombinu mingine zikiwemo reli na barabara za lami
zitakazounganisha maeneo ya vijiji vinavyozunguka Ikulu na mji wa
Serikali.
Pia
Mhe. Dkt. Magufuli amewahakikishia wananchi kuwa wote watakaoguswa na
shughuli za ujenzi wa miundombinu ya Serikali na wanaostahili kulipwa
fidia watalipwa, na ametoa wito kwa wananchi hao kutumia fedha za fidia
watakazolipwa kujenga makazi bora na kujipanga kufanya shughuli zenye
manufaa kwao.
“Hapa
sasa watakuja watu wengi, wafanyakazi na wageni maana tayari Mabalozi
wa nchi mbalimbali nao watajenga ofisi zao hapa, sasa na nyinyi mjipange
kufanya biashara, mtapata soko la kuuza mazao na bidhaa nyingine,
mkipata fedha ziwasaidie kwa manufaa na sio kuzichezea” amesisitiza Mhe.
Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema
utekelezaji wa Serikali kuhamia Dodoma unakwenda vizuri ambapo mpaka
sasa viongozi wakuu wa wizara zote na wafanyakazi 2,069 wameshahamia
Dodoma na wengine wanaendelea kuhamia Dodoma.
Mhe.
Majaliwa ameongeza kuwa atasimamia utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais
Magufuli aliyeagiza kujengwa kwa reli itakayounganisha eneo la Bwigili
na Dodoma mjini ili kurahisisha usafiri wa watu pamoja na kuharakisha
ujenzi wa barabara za kuzunguka mji wa Dodoma na barabara za kuunganisha
mji wa Serikali na Dodoma Mjini.
Wakiwa
katika eneo hilo, Mhe. Rais Magufuli na Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa
wameshiriki ufyatuaji wa matofali yatakayotumia katika ujenzi wa majengo
ya Ikulu.
Mapema
kabla ya kutembelea eneo hilo, Mhe. Rais Magufuli amepokea taarifa ya
mapendekezo ya ujenzi wa Mji wa Serikali wa Makao Makuu Dodoma kutoka
kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Mhandisi
Paskasi Muragili na kuagiza ujenzi wa Mji huo uzingatie maslai ya Taifa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
No comments:
Post a Comment