Akiwa amebakisha mechi sita za Ligi Kuu Bara sawa na dakika 540 za
kuichezea Simba, beki kiraka Abdi Banda amegomea saini ya miaka miwili
ya kuichezea timu hiyo.
Viongozi wa timu hiyo hivi sasa wanahaha kuipata saini ya beki huyo
pamoja na mshambuliaji wa timu hiyo, Ibrahim Ajib ambao mikataba yao
inamalizika mwishoni mwa msimu huu wa ligi kuu.
Banda alitua kuichezea Simba msimu wa 2015 kipindi hicho akiwa
anaichezea klabu ya timu ya vijana ya U20 (Ngorongoro Heroes) na Coastal
Union.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa kutoka kwenye
Kamati ya Utendaji ya timu hiyo, viongozi tayari wamemuandalia na kumpa
mkataba baada ya mazungumzo ya awali kufanyika lakini baadaye aligoma
kusaini.
Mtoa taarifa huyo alisema beki huyo amegoma kusaini mkataba wa mwaka
miaka miwili aliyopewa na viongozi wa timu hiyo huku yeye akiutaka wa
mwaka mmoja wa kuendelea kukipiga Simba.
Aliongeza kuwa uongozi wa timu hiyo unaendelea kufanya jitihada za
kuhakikisha wanamuongezea mkataba mwingine wa miaka miwili ya kuichezea
timu kwa kumpa dau zuri la usajili.
“Uongozi hivi sasa upo jitihada za kuhakikisha tunawasajili wachezaji
wote ambao mikataba nayo inamalizika mwishoni mwa msimu lakini kwa
vigezo maalum na kikubwa kikiwa ni kiwango na msaada na anaoutoa kwenye
timu, ”alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Banda kuzungumzia hilo alisema: “Nisingependa kulizungumza
hilo kwa hivi sasa kwani ninaogopa kujichanganya, hivyo tusubirie mechi
hizi sita nilizozibakisha zimalizike za ligi kuu ndiyo ntakuwa kwenye
sehemu nzuri ya kuongea.
“Naomba niishie hapo na kuhusu kitu kingine chochote kinachohusiana na
mkataba, basi aulizwe meneja wangu ataweza kuweka wazi kila kitu.”
No comments:
Post a Comment